WANAODAIWA KUMUUA DADA WA BILIONEA MSUYA WAONGEZEKA

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WATUHUMIWA wa mauji ya dada wa bilionea Erasto Msuya, Aneth Msuya wameongezeka baada ya mfanyabiashara
wa Arusha, Revocatus Muyela (40) kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji hayo.
Muyela alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwishoni mwa wiki na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Magreth Bankika.
Mshtakiwa anatuhumiwa kumuua dada wa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite bilionea, marehemu Erasto Msuya, Aneth Msuya.
Kupandishwa kizimbani kwa mfanyabiashara huyo kunafanya idadi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji hayo yaliyotokea Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, kufikia wawili baada ya kushitakiwa mke wa bilionea huyo, Miriam Msuya.
Mfanyabiashara huyo alisomewa shtaka la mauaji na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo.
Diana alidai mshtakiwa huyo, Mei 25 mwaka huu, eneo la Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, alimuua Aneth.
Mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji bali husikilizwa na Mahakama Kuu.
Wakili alidai upelelezi haujakamilika na kuomba kuahirishwa kesi hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.

No comments:

Post a Comment