Uda zaruhusiwa kusafirisha abiria wa Moshi, Arusha

Dar es Salaam. Hali tete ya usafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea mikoa ya Arusha na Kilimanjaro imeilazimu Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi kavu (Sumatra) kuomba mabasi 15 ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) ili kukabiliana na tatizo hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema jana wamelazimika kuomba mabasi ya Uda baada ya kubaini daladala za awali walizozipatia vibali haziwezi kukidhi mahitaji.
“Idadi ya abiria wanaokwenda Moshi imeongezeka ukizingatia kesho (leo) ni Sikukuu ya Krismasi, tutahakikisha wote wanakwenda baada ya kuongeza mabasi,” alisema.
Alisema wameagiza mabasi hayo yatoze nauli ya Sh 23,000 iliyopangwa na Sumatra.
Mkuu wa Mawasiliano ya Umma wa Uda, George Maziku alisema licha daladala hizo kufanya shughuli zake Dar es Salaam, wamelazimika kuzitoa ili kukabiliana na tatizo la usafiri lililowakumba wasafiri wa mikoa hiyo.
“Uda ni mali ya Watanzania hivyo si vibaya tukawasaidia wenzetu wanaokwenda kusherekea Sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya japokuwa Dar es Salaam nao wanahitaji huduma hii ya usafiri,” alisema Maziku.
Awadh Haji, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, alisema daladala hizo za Uda zilishakaguliwa.
Mmoja wa abiria, Chistopher Rafael aliyekuwa akielekea Moshi alipongeza jitihada za Sumatra za kukabiliana na tatizo hilo la usafri lililoibuka mwaka huu tofauti na miaka ya nyuma.
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Uda-zasafirisha-abiria-wa-Moshi--Arusha/-/1597296/2568562/-/11b559rz/-/index.html

No comments:

Post a Comment