Baadhi ya magari yanayopigwa picha njiani na raia wema na mabalozi wa usalama barabarani yakifanya makosa na picha zao kutumwa kituo cha mawasiliano cha kikosi cha usalama barabarani.
Baadhi ya magari yanayopigwa picha njiani na raia wema na mabalozi wa usalama barabarani yakifanya makosa na picha zao kutumwa kituo cha mawasiliano cha kikosi cha usalama barabarani
Na Augustus Fungo, Balozi wa Usalama Barabarani HIVI karibuni imejitokeza njia mpya ya kusaidia kupambana na wimbi la ajali za barabarani, ambapo pamoja na faini kwa madereva wanaokiuka sheria za barabarani wamekuwa wakipigwa picha na baadaye picha hizo kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii au magazetini na hata wakati mwingine kwenye televisheni. Mathalani katika mtandao wa facebook kundi la Mabalozi wa Usalama Barabarani maarufu kama, RSA wakishirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani hutumia mbinu hii kuwapiga picha wakiukaji wa sheria za barabarani kisha kuzituma katika Kituo cha Mawasiliano cha Usalama Barabarani (Traffic Control Center, TCC). Kituo hiki huwatumia picha hizi ambazo pia ni ushahidi askari waliopo katika vituo mbalimbali barabarani, ili kuwezesha watuhumiwa kukamatwa na magari husika. Baada ya kukamatwa magari husika askari humwandikia faini mkosaji, kumpiga picha na kuituma kwenye kituo cha mawasiliano ya polisi (TCC) ambacho na chenyewe hutoa mrejesho kwa watoa taarifa. Picha hizo hatimaye kuwekwa kwenye mtadao wa facebook, hutumika kuandaa vipindi vya televisheni vya kuelimisha jamii mfano, ni kipindi cha ‘Aibu yako' kinachorushwa na televisheni ya ITV na pia picha hizo huhifadhiwa na kikosi cha usalama barabarani kwa ajili ya kumbukumbu na rejea iwapo dereva husika atarudia kosa hilo. Njia hii mpya ambayo inaitwa kutaja na kuaibisha, ama kwa kiingereza “Naming and Shaming” ni maarufu sana inayotumika si tu na nchi nyingi za Ulaya bali pia na mashirika ya haki za binadamu kama 'Human Rights Watch', hutumia kuyaaibisha mataifa yaliyokubuhu kwa ukiukaji wa haki za binadamu. Saudi Arabia kupitia sheria yake ya makosa ya mtandao (Anti-cyber-crime law (Royal Decree No. M/17 dated 8 Rabi1 1428) imepitisha mbinu hii kama mojawapo ya adhabu. Mbinu kama hii hutumika pia katika nchi nyingi za Ulaya kuwaaibisha watu au makampuni yanayokwepa kodi. Moja ya makampuni yaliyowahi kuathirika na kadhia hii ni kampuni ya Kahawa ya Starbuck. Januari 15, 2015, serikali ya Uingereza iliwataja na kuwadhalilisha waajiri 37 wa Uingereza walioshindwa kulipa kima cha chini kwa wafanyakazi wao. Hata hivyo, mwandishi James Meernick(2012), anaitaja njia hii kama chaguo kuu la mashirika mengi ya kimataifa katika kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa. Njia hii hutumika ikiaminika kwamba kumuweka mtu au taasisi hadharani ili aweze kujiona mwenyewe, aonwe na familia yake, marafiki zake, na hata waajiri wakati akitenda kosa inasaidia kumfanya mtu ajitafakari na kutorudia kosa au pia kuwafanya wanaomzunguka kumpa shinikizo la kufuata sheria au kuheshimu haki za wengine.
Gari za serikali, mashirika ya umma, miradi, na zinginezo haziko juu ya sheria. Bila kujali operesheni wanayofanya au lengo la safari yao hawapaswi kuvunja sheria, na endapo watakuwa wamevunja sheria kwa sababu ya kwenda kuhudhuria dharula husika, askari aliyesimamisha hilo gari akiridhika na sababu hiyo hata toza faini wala kupiga picha, kwa hiyo hakuna kitakachoathirika. Na endapo kuna hofu ya matumizi mabaya ya hizo picha, atakaye wajibika ni huyo anayetumia vibaya picha hiyo ili mradi tu picha halisi (original) ya tukio zima ipo na ndiyo itakayotumika kama ushahidi dhidi ya mtu aliyeitumia picha vinginevyo. Ni ushauri wetu kuwa askari waendelee na mbinu hii ili wavunja sheria waaibike na kuweza kujirekebisha. Haiwezekani dereva amesomea amejaribiwa na kupewa leseni, anajua amebeba abiria kwenye gari lake halafu aendeshe kwa mwendo hatarishi, ayapite magari mengine kana kwamba amebeba viazi, au abiria ni mateka wake. Faini peke yake hazi saidii. Binafsi ningependa hata siku moja mahakama imhukumu mkosaji kufagia barabara za Kariakoo kwa wiki zima badala ya kumpeleka jela hii ingesaidia zaidi kurekebisha watu. Kimsingi ipo haja kama taifa tuwe na adhabu mbadala. Na kwa kuwa hakuna sheria inayovunjwa kwa mtu kupigwa picha wakati akitenda kosa na kuwekwa hadharani, mbinu hii bado itaendelea kuwa sahihi ili wahusika waache kutenda makosa ambayo yanagharimu si tu maisha ya watanzania bali pamoja na uchumi wa nchi. Naimani Jeshi la Polisi ni Jeshi lenye ueledi na wataalamu mbalimbali hivyo litaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kurekebisha tabia na kutekeleza sheria. Hii ndio imani yangu kwa taasisi hii muhimu nchini Tanzania, wananchi tushirikiane nao. Usalama Barabarani ni Jukumu Letu sote.
No comments:
Post a Comment