KAMANDA wa Polisi Kikosi Cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga, kwa kushirikiana na Kamishna Msaidizi wa Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Peter Sima, wameyadhibiti mabasi yaendayo mikoani katika stendi ya Ubungo yasipandishe nauli ambapo ulanguzi wa tiketi kwa abiria ulionekana kugonga mwamba.
Kamanda Mpinga na Kamishna Sima wametembelea ndani ya mabasi na kuuliza baadhi ya abiria juu ya nauli waliyolipia kama ndiyo sahihi kama iliyotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti, Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) huku wakisisitiza abiria kufunga mkanda na kutoa taarifa juu ya dereva anayeendesha gari kwa mwendo kasi.
Mpinga amesema, abiria yeyote atakayepandishiwa nauli tofauti na viwango vilivyotangazwa na serikari atoe taarifa kupitia namba maalum zilizotajwa kabla ya kuanza safari yao kuepuka mgogoro unaoweza kujitokeza wawapo safarini huku akizidi kusisitiza kuwa hakuna abiria atakayezidishiwa nauli kwa kipindi hiki cha sikukuu za Krismas na Mwaka mpya wa 2016.
Kwa upande wa askari wa vikosi vya barabarani (trafiki) Kamanda Mpinga amesema wamejipanga kuhakikisha askari wote wanakuwa na tochi maalum za kumulika magari yanayoendeshwa kwa mwendo kasi ili kupunguza hatari dhidi ya abiria.
(NA DENIS MTIM A/GPL)
No comments:
Post a Comment