Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizungumza katika kikao na Idara ya Misitu na Nyuki pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika ukumbi wa Ngorongoro Makao Makuu wa Wizara hiyo Mpingo House Jijini Dar es Salaam leo tarehe 05 Januari, 2015. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Mohammed Kilongo na Maofisa wa Misitu wa Mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya Serikali.
Akizungumza leo na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Wizara hiyo Dar es Salaam, Prof. Maghembe amesema agizo hilo limekuja kutokana na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.
Ameagiza pia maofisa hao wote wanaokusanya maduhuri ya Serikali katika Wilaya watumie muda wa siku kumi kuanzia leo kuhakikisha maduhuri yote yaliyokusanywa yanapelekwa benki ikiwa ni pamoja na kukabidhi vitabu vya kukusanyia mapato kinyume cha hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Wale district forestry officers wote wapeleke vitabu vyao wanavyokusanyia maduhuri ya Serikali kwenye ofisi za Kanda, Naibu Katibu Mkuu tusaidie kuwasiliana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali ifanye ukaguzi wa vitabu hivyo ndani ya siku kumi tuhakikishe fedha zinazotakiwa zinaingia kwenye mfuko wa Serikali, Mtu anakusanya fedha ya Serikali toka mwaka 2004 mpaka leo hajapeleka benki ananeemesha hali yake ya nyumbani, hili hapana”. Alisisitiza Prof. Maghembe.
No comments:
Post a Comment