Jipu kubwa hospitalini Mwananyamala

Mgonjwa akisaidiwa na ndugu yake.

Stori:Waandishi wetu, WIKIENDA DAR ES SALAAM:
Ikiwa ni moja ya kimbilio la mamia ya wagonjwa wengi jijini Dar kutokana na hadhi yake kuwa Hospitali ya Mkoa ya Mwananyamala, imekwaa madai mazito kwamba baadhi ya huduma si nzuri huku ucheleweshaji wa huduma hizo zikipigiwa kelele zaidi, Ijumaa Wikienda linatembea na wewe!
YALIKOTOKA MADAI
Kwa karibu wiki moja nyuma, baadhi ya ndugu wa wagonjwa na wagonjwa wenyewe, wamekuwa wakipiga simu kwenye chumba cha habari cha Global Publishers na kulalamikia mambo kadhaa katika huduma za hospitali hiyo ya rufaa.
MADAI YENYEWE
Watu hao walisema, kumekuwa na urasimu katika kutoa huduma ambapo mgonjwa anaweza kukaa mapokezi kwa muda wa saa nzima bila kuhudumiwa. Pia wakasema, wagonjwa wasiojiweza kutembea, huwekwa kwenye kiti cha magurudumu (wheel chair) na kuachiwa ndugu amsukume kwenda kwa daktari jambo ambalo walisema si sawasawa.
IMG_20160115_131033
Mgonjwa akiwa mapumzikoni.
“Kumsukuma mgonjwa kwa wheel chair pia kunataka uzoefu. Wakati mwingine msukumaji anajikuta akimgonga kwenye viti (benchi). Mimi ninavyojua, wahudumu ndiyo wanatakiwa kufanya kazi hiyo. OFM mje Mwananyamala mjionee, naona hili ni jipu kubwa,” alisema ndugu wa mgonjwa, aliyejitambulisha kwa jina la Songoro Mbina.
OFM KAZINI
Baada ya kupokea malalamiko hayo, timu ya Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM‘ ya Global Publishers, Ijumaa iliyopita, waliingia kazini ili kubaini kama madai hayo yana ukweli wowote. Ilibidi OFM wamtafute mgonjwa bandia.
KITENGO CHA MAPOKEZI
Wakiwa na ‘mgonjwa’ huyo aliyejifanya yuko hoi kwa ugonjwa usiojulikana, saa 6:22 mchana, OFM walifika hospitalini hapo wakiwa na Bajaj. Walimshusha mgonjwa huyo akiwa ‘amejilegeza’, lakini jambo la kushangaza hawakupata msaada wowote, hata kiti cha magurudumu kutoka kwa manesi, licha ya kuwepo katika eneo hilo.
IMG_20160115_124930
Wagonjwa wakiwa wamejilaza kwenye mabenchi.
MTOA HUDUMA MMOJA, WAGONJWA WENGI
OFM walimkokota mgonjwa wao mpaka mapokezi na kubaini mtu anayetoa huduma ni mmoja licha ya kuwepo wagonjwa wengi waliokuwa wakihitaji huduma kutoka kwake.
Mtoa huduma huyo pia alikuwa akiandikisha kadi kwa wagonjwa wapya na kupokea malipo ya wagonjwa waliotakiwa kufanyiwa vipimo baada ya kutoka kwa daktari.
WAGONJWA WALALA KWENYE MABENCHI
OFM iliendelea kushuhudia mengine ya kushangaza kwa hospitali kubwa kama Mwananyamala. Madirisha mawili yaliyotakiwa kuwa na wahudumu yalifungwa hivyo kumpa kazi nzito mhudumu huyo mmoja.
Mbali na upungufu huo, OFM walishuhudia baadhi ya wagonjwa wakiwa wamelala kwenye mabenchi ya mapokezi wakisubiri foleni kupungua ili waweze kuhudumiwa.
NDUGU WA MGONJWA ANENA
“Aisee, hii ni hatari! Mgonjwa wangu ana hali mbaya, nimekwenda ‘emergency’ wamesema hawawezi kumpokea bila kadi. Kwa foleni hii sijui atatibiwa muda gani!” alilalama mtu mmoja aliyempeleka mgonjwa.
IMG_20160115_124154ANGALIA SASA
OFM iliandikisha kadi na kumuweka mgonjwa wao kwenye kiti cha magurudumu. Walimsukuma wenyewe kuelekea chumba cha daktari walikokuwa wameelekezwa. Pia baadhi ya wagonjwa walikuwa wakiwasukuma wagonjwa wao kwenye viti hivyo. Hiyo ilikuwa saa 7:17 mchana.
Kutokana na wingi wa wagonjwa kwenye chumba cha kwanza, cha pili na cha tatu, alitokea nesi mmoja aliyewaambia OFM waende chumba cha huduma ya haraka (OPD & Emergency).
Madaktari wa huko walianza kumhudumia ambapo mmoja alisema mgonjwa wa OFM alionekana kuwa na kisukari kwa hiyo alitakiwa kufanyiwa vipimo haraka.
APEWA DAWA BILA KUFANYIWA VIPIMO
Bila ubishi, mmoja wa OFM alikwenda kushughulikia malipo ya vipimo vya kisukari lakini baada ya kukamilisha na kurudi emergency, alikuta mgonjwa amehamishiwa kwenye chumba cha saikolojia na alishapewa dawa ambazo daktari alisema ni za kisukari, zimeandikwa benzhexol.
DAWA NUSU NDANI, NUSU NJE
Hata hivyo, dawa hizo zilikuwa nusu ambapo mtu wa duka la dawa alisema zilibaki hizo na kutakiwa kwenda kununua nyingine kwenye maduka ya dawa yaliyopo nje ya hospitali hiyo.
MAENEO MENGINE
Hata hivyo, vitengo vingine vilikuwa sawa, mfano kwenye X-ray na vyumba vya ndani, wauguzi waliovaa suruali nyeupe na mashati meupe, walikuwa wakipokea wagonjwa kwa unyenyekevu na maelekezo ya kuridhisha huku wakitumia lugha ya ubinadamu.
Saa 8:43, OFM waliondoka hospitalini hapo wakiwa wamekamilisha uchunguzi wake.
MGANGA MKUU ANENA
Baada ya OFM kumaliza kazi hiyo iliyochukua kama saa 2, iliondoka hospitalini hapo na siku iliyofuata ilimtafuta mganga mkuu wa hospitali hiyo, Delila Moshi na kuelezewa malalamiko ya wagonjwa na ukaguzi wa OFM ulivyofanyika ambapo alisema:
“Kwanza ni muda gani mmefanya huo uchunguzi wenu? (akaambiwa). Lakini hata hivyo, malalamiko nimeyasikia, ila siwezi kuzungumza kwa kuwa sina data za kutosha juu ya ukweli wa hayo.
“Mimi ningeomba sana mnifahamishe siku na saa ili niwajue wahusika waliokuwepo zamu na niweze kulishughulikia suala hilo.”
Waandishi: Boniphace Ngumije, Andrew Carlos, Nyemo Chilongani, Mayasa Mariwata na Suzane Kayogela.

No comments:

Post a Comment