Kwa hali hii Nchi inaliwa!

Makongoro oging’, AMANI

DAR ES SALAAM: Da! Wakati Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’ akiendelea kutumbua majipu kwa vigogo mbalimbali serikalini, hasa wanaotuhumiwa kwa ufisadi, Amani limenasa vigogo wengine wanne wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao wamejenga mahekalu ya mabilioni ya shilingi huku wakiishi maisha ya juu kama ‘miungu watu’, kweli nchi inaliwa! Awali, mahekalu mengine yaliyosemekana kuwa ni ya vigogo wa mamlaka hiyo, yalinaswa na kutolewa kwenye gazeti hili.
CHANZO CHAZUNGUMZA NA AMANI
Mapema wiki hii, chanzo chetu cha habari kilifika kwenye ofisi za gazeti hili na kuonana na wahariri wa Global Publishers kulalamikia maisha ya baadhi ya vigogo wa TRA kwamba ni ya anasa sana wakiwa wanaishi kwenye mahekalu (majumba) ya kifahari huku Watanzania walio wengi wanaishi kwa mlo mmoja tena kulala kwa kubanana.
MSIKIE MWENYEWE
“Jamani ndugu zangu, lengo la mimi kuja hapa ni kutaka kuwaambia kwamba, kuna vigogo wa TRA wanaishi Mbezi Beach. Wamejenga majumba ya kifahari. Wanamiliki magari ya kisasa, lakini najua pesa zao ni za ufisadi.
“Nimekuwa nikifuatilia kwenye vyombo vya habari ili kuona kama kuna siku watawekwa hadharani lakini wapi! Naamini serikali haijawajua. Wale wakifuatiliwa, watabainika namna walivyoitafuna hii nchi na ndiyo maana wanaishi kwa kuabudiwa hata na viongozi wa serikali ya mtaa.”
KWENYE VIKAO WANATUMA WAWAKILISHI
“Sisi wenye vijumba vya kujenga miaka saba havijaisha tunajisikia vibaya sana. Ni majirani zetu lakini hatuonani. Wakitoka nje ya mageti yao wamo ndani ya magari yenye tinted. Wananuka pesa hata familia zao. Wanaogopwa mtaani.
“Siku kukiwa na kikao cha serikali ya mtaa kuzungumzia mambo ya maendeleo wanatuma wadogo zao, shemeji zao, wengine wanatuma hata mahausigeli. Hivi ni haki kweli jamani?!”
IMG_1414KUONEKANA KWAO
“Mimi nimewahi kuwaona wawili tu kwa nyakati tofauti, walikuwa wana shida kwenye ofisi za serikali ya mtaa. Kusema ule ukweli nchi hii inaliwa sana. Kama kila mmoja angefanya mambo kulingana na kipato chake halali, taifa lingekuwa mbali sana. Lakini watu wanaiibia serikali kwa ajili ya kujitajirisha na familia zao,” alisema mtoa habari huyo.
KUNA DOGO WA MIAKA 27 NAYE
Wakati mtoa habari wetu akihitimisha hivyo, vyanzo vingine vya habari vimesema kuwa, kijana wa miaka 27 (jina linahifadhiwa kwa sasa), mfanyakazi wa kawaida (kama ‘mfagizi’) wa TRA anamiliki jumba la kifahari lenye vyumba vya kulala 10, sebule 2, vyoo vya umma vitatu, sehemu ya kulia chakula 2 huku msingi wa nyumba ukiwa na urefu wa nyumba nyingine.
“Huyu dogo ana miaka kama 27 tu, lakini anamiliki jengo la kifahari huko Goba. Maisha yake kwa ujumla ni ya kutumbua raha. Kumbe hawa jamaa wa TRA wana pesa sana. Mimi sikuwahi kufikiria. Sasa kwa nini walimu na polisi wanahangaika namna hii?” alihoji mtoa habari wetu.
AMANI LASAKA UKWELI
Baada ya kunyetishiwa ubuyu huo, mapaparazi wetu walizama mtaani ili kujiridhisha. Ilibidi mapaparazi wetu wamtafute Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach, Pantaleo Mushi ambaye alikiri kuwa, baadhi ya nyumba katika eneo hilo ni za wafanyakazi wa TRA.
“Ni kweli baadhi ya nyumba za mtaa wangu ni za watu wa TRA, lakini hayo mengine siyafahamu kabisa. Ila kama mnataka kujua zaidi, nendeni wenyewe. Maisha ya watu ni utaratibu wao wenyewe, wanavyoishi ni vile watakavyo,” alisema.
Amani: “Vipi lakini, kukiwa na vikao vya serikali za mtaa wanajitokeza?”
Mwenyekiti: “Wanafika…wanafika.”
Amani: “Mbona tunasikia wanatuma wawakilishi?”
Mwenyekiti: “Labda wanapokuwa na udhuru.”
land-rover-range-rov-8_1600x0wMfano wa mikoko wanayomiliki.
KIJANA NA AMANI
Baada ya kuzungumza na mwenyekiti huyo, juzi, saa 5:28 asubuhi, gazeti hili lilimpigia simu kijana huyo ambapo baada ya mwandishi kujitambulisha jina na chombo cha habari, alikata simu.
ILIVYOKUWA IKIJULIKANA
Baadhi ya watu waliozungumza na Amani kuhusu vigogo wa TRA kujenga majumba ya kifahari maeneo ya Mbezi Beach walisema kuwa, awali waliamini kwamba, nyumba za maeneo hayo nyingi ni za wafanyabiashara na Wazungu waliweka makazi yao nchini.
“Jamani mimi nilipokuja kugundua kwamba, waliojenga Beach wengi ni jamaa wa TRA, TRL (Shirika la Reli Tanzania) na TPA (Mamlaka ya Bandari Tanzania), nilishangaa sana, zamani nilijuwa ni wafanyabiashara wakubwa na Wazungu wanaoishi nchini,” alisema Hamud Hassan Lukwu, mkazi wa Mbezi.
Akizungumza na wakazi wa Ngarenaro jijini Arusha hivi karibuni akiwa njiani kuelekea kwenye Kambi ya Jeshi Monduli, JPM alisema kuwa, mpango wake wa kutumbua majipu viongozi wa serikali ambao wanatumia pesa za umma kwa manufaa binafsi utaendelea mpaka watakapokwisha wote.
mercedes-benz-cls-class-01TAKUKURU WATOA NENO
Akizungumza na wanahabari jijini Dar juzi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Valentino Mlowola alitoa onyo kwa taasisi nyeti nchini, zikiwemo zinazohusika na matumizi ya fedha za umma kufuata sheria, taratibu na kanuni.
Mlowola alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kwa wananchi kuwajulisha matendo ya rushwa na ufisadi yanayoendelea hapa nchini.
Alisema kutokana na hali ya wananchi kuona nia ya serikali ya awamu ya tano katika kushughulikia matatizo ya rushwa na ufisadi ametoa onyo kwa maofisa wa umma wanaofanya rushwa na ufisadi kuwa sehemu yao ya kazi na miradi ya kuwaingizia kipato kuacha mara moja.

No comments:

Post a Comment