Marehemu Clara Justin Munishi enzi za uhai wake.
Stori: Makongoro Oging’, UWAZI
DAR ES SALAAM: Dunia katili! Clara Justin Munishi (30), mkazi wa Keko Mwanga, Temeke jijini Dar amefariki dunia baada ya kudaiwa kupigwa na kujeruhiwa vibaya na mumewe, Novatus Peter Kabero.
Tukio hilo la kikatili, lilitokea usiku wa saa tano, Januari 13, 2016 nyumbani kwa wanandoa hao ambapo kwa mujibu wa majirani, mwanamke huyo alisikika akilia na kuomba msaada kwa muda mrefu kutokana na kushushiwa kipigo kikali na mumewe.
Mume wa marehemu Novatus Peter Kabero.
“Unajua hawa ilikuwa kama kawaida yao kugombana, mara kwa mara mwanaume alikuwa akimpiga sana mkewe hasa nyakati za usiku. Sasa siku hiyo hata tuliposikia Analia na kuomba msaada, tulijua ni kama kawaida yao, kumbe mwenzetu alikuwa anauawa,” alisema mwanamke mmoja anayeishi jirani na eneo la tukio, aliyekataa kujitambulisha jina lake.
Habari zaidi kutoka kwa vyanzo vyetu, zinaeleza kuwa baada ya kuzidiwa na kipigo, mwanamke huyo aliyekuwa na ujauzito wa miezi mitatu, alidondoka na kupoteza fahamu, mumewe akaendelea kumpiga kisha akamburuza na kumtoa nje ya uzio alikomtelekeza na kutokomea kusikojulikana.
Waombolezaji wakiwa msibani.
“Ilibidi jirani mmoja apige simu polisi kwa sababu siku hiyo alikuwa akilia sana tofauti na siku zote anazopigwa na mumewe. Pia tulishindwa kwenda kuwaamulia kwa sababu mumewe ana kawaida ya kuwatishia watu na bastola. Muda mfupi baadaye, polisi walifika eneo la tukio, wakamchukua akiwa hajitambui na kumpeleka Hospitali ya Temeke ambako alifariki dunia muda mfupi baadaye.
Ndugu wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Raymond Kavishe, aliliambia Uwazi kwamba wamesikitishwa sana na kifo cha kinyama cha ndugu yao na kuliomba jeshi la polisi kumsaka mtuhumiwa ili sheria ichukue mkondo wake.
Mwili wa marehemu ulisafirishwa Jumatano ya wiki iliyopita kwenda kijijini kwao, Marumumlama, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro alikozikwa Alhamisi ya Januari 21, mwaka huu. Marehemu ameacha mtoto mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Andrew Satta alipoulizwa, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa chanzo cha mauaji hayo, inadaiwa ni mwanamke huyo kukaidi amri ya mumewe aliyemkataza kwenda kwa rafiki wa marehemu kwa madai kwamba anamtafutia wanaume. Kamanda Satta aliongeza kwamba mtuhumiwa anaendelea kusakwa na jeshi la polisi kwani alitoroka baada ya kufanya mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment