Rombo. Wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro imetajwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa uingizwaji wa silaha kiholela nchini, hali inayochangia ongezeko la uhalifu.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na madiwani na uongozi wa wilaya hiyo.
Alisema matukio mengi ya uhalifu yanayotokea hufanywa na baadhi ya watu kutoka nchi jirani ya Kenya kwa kushirikiana na Watanzania.
“Kamati ya ulinzi na usalama inawataka mdhibiti uingizwaji holela wa silaha hizo, sitaki wilaya iwe kitovu cha uhalifu,” alisema Makala.
Pia, alisema Serikali haitawavumilia askari watakaobainika kushiriki katika suala la kuingiza wahamiaji haramu.
Akizungumzia mapato, aliwataka madiwani kubuni vyanzo vya mapato vitakavyosaidia kuongoza pato na kukuza uchumi.
“Kati ya halmashauri ninazozishangaa ni pamoja na hii ya Rombo... mpo mpakani lakini mapato yenu hayaridhishi,” alisema.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Evarist Silayo alisema madiwani wameweka sheria ndogondogo za ukusanyaji wa mapato zitakazosaidia kuongeza pato la halmashauri.
No comments:
Post a Comment