Machangudoa wakiwa kwenye mawindo.
Erick Evarist na Richard Bukos, RISASI mchanganyiko
DAR ES SALAAM: Licha ya jitihada za serikali kutangaza vita dhidi ya wauzaji na wanunuzi wa miili ya kinadada na kuwataka waache kwa kuwa ni kinyume cha maadili na sheria ya nchi, warembo hao (sio walio pichani ukurasa wa nyumawamedaiwa kukaidi agizo hilo huku wakidai kama aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba alishindwa basi hata mkuu mpya wa mkoa huo, Paul Makonda hatawaweza.
Hivi karibuni, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Simon Sirro alitangaza oparesheni maalum ya kuwasaka madada poa hao, sambamba na wateja wao akidai wanakiuka sheria na maadili ya Mtanzania jambo ambalo liliungwa mkono na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
….Wakiikimbia kamera.
Mara baada ya agizo hilo la serikali kutolewa, wanahabari wetu walifanya uchunguzi katika maeneo ambayo yamezoeleka kwa biashara hiyo na kukuta baadhi yao wakiendelea kama kawaida kana kwamba hakuna agizo lolote lilitolewa.
Risasi lilipita maeneo ya Sinza-Mori jijini Dar na kuwakuta akina dada hao wakiendelea na biashara hiyo kwa kujipanga barabarani kuelekea baa maarufu ya Meeda ambapo wanahabari wetu waliojifanya wateja walipowauliza kulikoni hawaogopi nguvu ya dola, walisema wao wameshindikana tangu enzi za Makamba, Kandoro na Said Meck Sadick (aliyepita) hivyo hata huyu wa sasa, Makonda hatawaweza.
“Wewe hii ni nguvu ya soda. Hatuwezi kuacha unafikiri tutakula wapi? Hii kazi tumeanza kitambo, tangu enzi za Makamba aliyekuwa hatari kweli kukemea biashara hii lakini tulimshinda. Akaja Sadick naye tukamgaragaza sembuse huyu Makonda aliyepewa jiji hili juzi tu?” alisema dada poa mmoja aliyekataa kutaja jina lake.
Maeneo mengine ya Jiji la Dar ambayo Risasi lilibaini kuwa biashara hiyo bado inaendelea kama kawaida ni pamoja na Sinza-Afrikasana (maarufu kama Conner Bar), Buguruni (Kimboka Bar, Rozana), Temeke na Kinondoni-Makaburini.
Alipotafutwa Makonda kuhusiana na suala hilo alisema atalizungumza kwa kirefu baada ya Sikukuu ya Pasaka lakini mwanahabari wetu alipombana zaidi ili aweze kutoa ufafanuzi kwa kuwa madada poa hao wamekaidi agizo la serikali, aliahidi kulizungumzia siku iliyofuata (Machi 21) lakini hata hivyo siku hiyo alipopigiwa simu hakupokea.
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda.
Hata mwandishi wetu alipomtumia ujumbe mfupi wa maandishi kumsisitiza azungumzie suala hilo, Makonda hakujibu chochote.
Aidha, mwandishi wetu pia alimtafuta Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro ili aweze kuzungumzia suala hilo, aliomba atafutwe baadaye kwa kuwa alikuwa kwenye kikao. Baadaye simu yake haikupatikana hewani.
No comments:
Post a Comment