Rais Magufuli akisalimiana na baadhi ya viongozi wa serikali na wageni waliofika kwenye uzinduzi huo.
Rais Magufuli akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dar, Paul Makonda mara baada ya kuwasili.
Rais Magufuli akiwasili.
Viongozi wakijiandaa kumpokea rais Magufuli.
Umati wa watu waliofika kushuhudia tukio la uzinduzi wa Daraja la Kigamboni leo.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Kijazi akiwasili.
Taswira ya daraja hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli akikata utepe huku viongozi wengine wakiushikilia kuashiria uzinduzi rasmi wa Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016.
(PICHA NA DENIS MTIMA)
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli akikata utepe huku viongozi wengine wakiushikilia kuashiria uzinduzi rasmi wa Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli na viongozi wengine wakitembea juu ya Daraja la Kigamboni baada ya kulizindua katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Magufuli leo amezindua rasmi Daraja la Kigamboni lenye urefu wa mita 680 ambalo limejengwa juu ya Bahari ya Hindi kuunganisha kata za Kigamboni na Kivukoni.
Katika hafla ya uzinduzi huo, rais Magufuli amesema kuwa, daraja hilo lisiitwe ‘Daraja la Magufuli’ na badala yake amependekeza lipewe jina la muasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyewaunganisha Watanzania bila kujali itikadi ya vyama, dini, kabila wala rangi.
Akiongea wakati wa kuzindua daraja hilo leo, Rais Magufuli amesema kuwa awali aliletewa mapendekezo na waziri mwenye dhamana akimtaka aridhie daraja hilo lipewe jina lake, lakini kwakuwa wazo la ujenzi huo lilianza tangu wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, alikataa na kushauri jina la Nyerere litumike.
“Nilikataa lisiitwe kwa jina langu kwa sababu wazo la ujenzi wa daraja hili lilianza mwaka 1979 wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere.
“Wazo hilo halikufanikiwa kutokana na ukosefu wa pesa wakati huo. Mwalimu Nyerere ni kiongozi aliyejenga misingi imara katika taifa letu.
“Alikuwa ni kiongozi asiyebagua mtu kwa misingi ya dini, chama au kabila. Alifanikiwa kutuunganisha watanzania wote bila kujali itikadi zetu.
“Leo hii, daraja hili limekamilika, ni daraja ambalo halitambagua mtu kwa sababu wa CCM watapita hapa, wa Chadema watapita hapa na bahati nzuri mstahiki Meya wa jiji hili ambaye ni Chadema naye yuko hapa na amepita katika daraja hili.
“Ndugu zangu sistahili sifa zozote, najua nimefanikisha ujenzi huu nikiwa waziri wa ujenzi, lakini wakati huo nilikuwa natimiza wajibu wangu kama mtumishi wa umma, hivyo nashauri hili daraja liitwe daraja la Nyerere ili tuweze kumuenzi mwasisi wa taifa hili” alisema Rais Magufuli.
Mbali na hilo, rais Magufuli pia hakusita kuzungumzia suala la kulipisha wananchi watakaokuwa wanavuka kwa kutumia daraja hilo na kusema kuwa, watakaopita kwa gari, pikipiki na baiskeli lazima walipie (jpo hakutaja kiwango watakachotakiwa kulipia) na kwamba wataendelea kulipia mpaka pale ambapo tamko jingine utakapotolewa wakati huo waenda kwa miguu hawatalipia, watapita bure. Akaongeza kuwa tozo hiyo itasaidia kuongeza kipato kitakachotumika kujenga daraja lingine kama hilo.
Akiendelea na kuhutubia, Rais Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Bw. Wilson Kabwe kutokana na ufisadi katika utekelezwaji wa mikataba mitatu, inayohusu maeneo ya ukusanyaji mapato ya Stendi Kuu ya Mabasi Yaendayo Mikoani ya Ubungo na kodi ya uegeshaji magari katikati ya jiji na kuisababishia serikali hasara ya pesa zaidi ya bilioni 3.
Daraja la Kigamboni limejengwa katika mkondo wa Kurasini (Kurasini Creek), mradi huu uliobuniwa na Arab Consulting Engineers na kujengwa na wakandarasi kampuni za China Railway Jiangchang Engineering (T) Ltd na China Major Bridge Engineering Company, unamilikiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Aidha Rais Magufuli amewataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanalitunza daraja hilo katika kujenga uchumi wa Taifa.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 19 Aprili, 2016 amefungua rasmi Daraja la Kigamboni linalounganisha usafiri wa barabara kati Kigamboni na Kurasini Jiji la Dar es salaam na amependekeza Daraja hilo liitwe Daraja la Nyerere (Nyerere Bridge).
Sherehe za ufunguzi wa daraja hilo kubwa na la kipekee kwa Afrika Mashariki na Kati zimefanyika kando ya daraja hilo upande wa Kigamboni na kuhudhuriwa na viongozi na wageni mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. Lu Youqing, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhandisi Edwin Ngonyani, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) Mheshimiwa Antony Mavunde, Wabunge na Mameya wa Jiji na Dar es salaam.
Ujenzi wa daraja hilo umehusisha nguzo mbili za pembezoni na mihimili miwili inayoshikilia nyaya 36, na daraja zima lina urefu wa meta 680, upana wa mita 32, njia sita za magari, njia mbili za watembea kwa miguu na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5.
Daraja hilo limejengwa kwa fedha za ndani na kugharimu jumla ya shilingi Bilioni 254.12 ambapo kati ya fedha hizo asilimia 60 zimetolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), na asilimia 40 zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Kujengwa kwa Daraja hili kutaondoa kero ya msongamano wa magari na usafiri kwa wakazi wa Kigamboni na wakazi wa katikati ya Jiji la Dar es salaam ambao walilazimika kutumia kivuko (Ferry) ili kukatiza eneo la mkondo wa bahari ya Hindi ama kutumia barabara ya kuzunguka kupitia Kongowe lenye urefu wa kilometa 52.
Daraja hilo limefanyiwa majaribio kwa kutumia Malori 44 yenye uzito wa tani 30 na limethibitika kuwa na uwezo wa kubeba jumla ya tani 1,320 na hivyo linatarajiwa kusaidia usafirishaji wa mizigo ya kutoka na kuingia katika bandari ya Dar es salaam.
Akizungumza katika sherehe hizo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza vyombo husika vianze mchakato wa daraja hilo kupewa jina la “Daraja la Nyerere” (Nyerere Bridge) ikiwa ni kuuenzi mchango mkubwa wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefanya kazi kubwa ya kuijenga Tanzania.
Aidha, Rais Magufuli amewapongeza wadau wote waliohusika kufanikisha ujenzi waDaraja hilo likiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na wakandalasi kutoka China, na ametaka watanzania wajivunie daraja hilo kubwa na lililojenga heshima kubwa kwa nchi.
Pia Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa vyombo vya habari vya Tanzania kuitangaza vyema Tanzania na kuwa na uzalendo wa kweli kwa nchi yao badala ya kubeza kazi nzuri zinazofanywa ndani ya nchi kwa manufaa ya watanzania.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bw. Wilson Kabwe na kuagiza vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili za kusaini mikataba iliyosababisha serikali kupoteza mapato.
Dkt. Magufuli ametangaza uamuzi huo wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa daraja la Kigamboni, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Makonda kumueleza kuwa amebaini upotevu wa shilingi Bilioni 3 uliotokana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Bw. Wilson Kabwe kusaini mikataba ya ukusanyaji mapato ya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kwa kutumia sheria iliyopitwa na wakati, na pia ukusanyaji wa tozo za uegeshaji wa magari ndani ya Jiji.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
19 Aprili, 2016
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
19 Aprili, 2016















No comments:
Post a Comment