Kinyozi auawa kwenye fumanizi

msangiKamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza SACP Ahmed Msangi
Na Mashaka Baltazar, AMANI
MWANZA: Fundi wa kunyoa nywele (kinyozi) aliyetajwa kwa jina moja la Idd (35), mkazi wa Kijiji cha Kome, Kata ya Bukiko kilichopo katika Kisiwa cha Ukerewe, ameuawa kwenye madai ya fumanizi na mke wa Bagaile Ndaro nyumbani kwa mwenye mke huyo.
Mauaji hayo yalijiri Juni 18, mwaka huu, saa 1:00 usiku. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Ndaro kwa mahojiano huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea. Marehemu huyo aliuawa kwenye fumanizi hilo baada ya kushambuliwa na kundi la watu waliokuwa na silaha za jadi za ncha kali pamoja na mawe hadi akapoteza maisha baada ya kumfumania akifanya ngono na mke wa Ndaro nyumbani kwake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza SACP Ahmed Msangi alisema marehemu kabla ya kuuawa kwa kupigwa mawe na vitu vyenye ncha kali, alifumaniwa nyumbani kwa mgoni wake (Ndaro) akifanya ngono na mkewe Fodia Colnelius.
Kitendo hicho kilimuudhi Ndaro hivyo akaamua kumshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake akishirikiana na kundi la watu waliofika kwenye tukio hilo hadi wakamuua kinyozi huyo.
“Marehemu aliuawa baada ya kufumaniwa ndani ya nyumba ya mgoni wake akiwa anafanya ngono na mkewe Fodia Colnelius (mke wa Ndaro). Kitendo hicho kilimuudhi mwenye mke na kusababisha amshambulie Idd kwa mawe, vitu vyenye ncha kali akishirikina na kundi la watu wengine na kusababisha kifo cha kinyozi huyo,” alisema Kamanda Msangi.
Msangi aliongeza kuwa kutokana na mauaji hayo ambayo chanzo chake ni ugoni polisi wanamshikilia mwenye mke kwa mahojiano akituhumiwa kushiriki mauaji hayo ambapo msako wa kuwatafuta washirika wake unaendelea na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Kamanda huyo alieleza kuwa jeshi hilo limekuwa likisisitiza wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi badala yake watii sheria bila shuruti pindi wanapowakamata watuhumiwa watoe taarifa kwa jeshi hilo au wawapeleke kwenye vituo vya polisi kwa hatua za kisheria.
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Wilaya ya Magu linamshikilia Futa Bujilima (38) mkazi wa Kijiji cha Mwabulenga kilichopo Kata ya Ng’haya Tarafa ya Ndagalu katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba ya hawara yake Lucia Andrew (40).
Katika tukio hilo lililotokea Juni 18, mwaka huu majira ya saa 4:00 usiku katika kijiji hicho nyumba hiyo pamoja na vitu vyote vilivyokuwemo ndani kuteketea kwa moto huo huku mtoto mwenye umri wa miaka 6, Vumilia Lufungulo akijeruhiwa usoni na kwenye shavu la kushoto.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Lucia ambapo siku hiyo ya tukio alikwenda nyumbani hapo na hakumkuta hivyo akahisi alikuwa amekwenda kwa wanaume wengine ndipo akachukua uamuzi wa kuichoma nyumba yake kwa moto.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi (pichani) alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mtuhumiwa anashikiliwa wakati upelelezi ukiendelea kabla ya kufikishwa mahakamani ambapo majeruhi amelazwa katika Kituo cha Afya cha Kabila kwa matibabu huku hali yake ikiendelea vizuri.

No comments:

Post a Comment