KESI ya madai iliofunguliwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kuiomba mahakama kupiga marufuku zuio la Polisi, leo limetupiliwa mbali.
Mbowe alifungua kesi hiyo namba 79 ya mwaka 2016, baada ya hivi karibuni Jeshi la Polisi kupiga marufuku mikutano ya hadhara kwa madai kwamba, hali ya usalama nchini si salama.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, Kilimanjaro katika shauri hilo, aliwashtaki Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kwa madai wanahusika kuzuia kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Mbowe ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, walitangaza kufanya oparesheni iliopewa jina ‘Okoa Demokrasia nchini’ iliyokuwa na lengo la kuishtaki serikali kwa wananchi kwa kile alichodai, kuendesha nchi bila kufuata katiba ya nchi.
Hata hivyo, baada ya kupigwa marufuku kwa maandamano, Mbowe alifungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, akiiomba kutengua zuio hilo la polisi.
Mohammed Gwae, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, leo amepitia ombi lililopelekwa mahakamani hapo na upande wa mlalamikaji anayewakilishwa na mawakili John Mallya na Gasper Mwanalelya na kutoa uamzi.
Jaji Gwae akitoa uamuzi wa ombi la walalamikaji amedai kuwa, amefikia hatua hiyo baada ya walalamikaji kukosea kifungu cha kupeleka shauri hilo kortini kitendo kilichosababisha kulitupilia mbali.
Amesema kuwa, walalamikaji baada ya kupeleka ombi hilo kortini, upande wa wajibu maombi unaoongozwa na mawakili, Seth Mkemwa na Robert Kidando waliweka pingamizi wakiomba mahakama kutokusikiliza ombi hilo.
Jaji Gwae amesema kuwa, walalamikaji katika ombi lao walikosea kutumia kanuni ya tano kifungu kidogo cha tatu cha sheria ya mwaka 2014 badala ya kanuni ya tano kifungu kidogo cha pili ambacho kilitakiwa kutumiwa.
“Waleta maombi wametumia kanuni ya tano kifungu kidogo cha tatu badala ya kutumia kanuni ya tano kifungu kidogo cha pili kilichotakiwa kuwepo katika kuleta ombi na kama kifungu hiki hakijatumika hapo na ombi halipaswi kupokelewa,” amesema Jaji Gwae.
Hata hivyo Jaji Gwae amesema, licha ya kuwekewa pingamizi na wajibu maombi, walalamikaji wamesema kanuni na kifungu hicho ndivyo vilitakiwa kuwepo na hivyo vinavyopaswa kuwekwa sio sahihi.
Amesema kuwa, katika shauri la namna hiyo, kanuni na vifungu vilivyotakiwa kuwepo ni kanuni ya tano kifungu kidogo cha pili na kanuni ya tano na kifungu kidogo cha vya sheria ya mwaka 2014 na kwamba wao waliviweka katika maelezo (Statements) badala ya (chember samers).
Mallya, mwanasheria wa mpeleka maombi amesema kuwa, baada ya kukosea kanuni na vifungu hivyo, watapeleka kwa mara nyingine ombi na kulifanyia marekebisho kama Jaji Mohamed Gwae alivyoelekeza.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment