Mume: Bosi bandari kanipora mke

mume (1)Kherry Temba
Stori:BONIPHACE NGUMIJE
DAR ES SALAAM: Kherry Temba, mkazi wa Mbagala jijini Dar, ameibuka na kumtuhumu mmoja wa mabosi wa bandari ya Kigoma (jina tunalihifadhi) kuwa amempora mkewe, Lilian Milanzi hadi kufikia hatua ya kumvunjia ndoa yake.
Temba amedai kuwa walioana na Lilian kwa ndoa halali Mei 28, 2010 katika Kanisa la Azania Front jijini Dar ndipo baadaye kigogo huyo wa bandari alipomrubuni.
mume (2)Kherry Tembaakiwa na mkewe siku ya ndoa yao.
Alisema baada ya kuoana walifurahia maisha ya ndoa, wakafanikiwa kupata mtoto mmoja. Ilipofika mwaka 2014 ndipo Lilian alipounganishwa na baba yake mzazi aliyekuwa akifanya kazi Bandari ya Dar, kwenda kukutana na kigogo huyo wa Kigoma ambaye alitumia fursa hiyo kumrubuni.
Temba alizidi kudai kuwa, bosi huyo alifanikiwa kumpata Lilian baada ya kumsaidia kibarua katika bandari hiyo.
“Yaani jamaa (bosi) alitumia madaraka vibaya, akanipora mke wangu, mke wangu naye akakubali kudanganyika, basi na mimi sikuwa na jinsi, nimemuachia Mungu,” alisema mwanaume huyo.
Aliendelea kusema kuwa baada ya kufanikiwa kumpa kazi hiyo, mke alilazimika kuhamia Kigoma na kumuacha yeye jijini Dar, wakawa na utaratibu wa kila mmoja kwenda kuishi kwa muda kwa mwenzake lakini mwaka jana ndipo alipogundua kuwa anaibiwa mkewe.
“Nilienda kumtembelea Kigoma, nikatonywa kuwa naibiwa. Kama hiyo haitoshi, nikashuhudia gari la bosi limemletea maji mke wangu nyumbani jambo ambalo ni gumu kwa mfanyakazi wa chini kama yeye.
“Nilipomuuliza mke wangu akawa mkali ndipo vitimbi vilipoanza. Tukawa tunagombana hadi tukafikia hatua ya kuachana, mke wangu hakutaka hata kurudi tena nyumbani kwetu Mbagala, akamtuma dada yake kuja kumchukulia nguo zake,” alisema Temba.
Alipotafutwa Lilian na kusomewa tuhuma hizo, alikanusha na kusema mumewe huyo ndiye mkorofi kwani amekuwa akimhisi mambo ambayo hayafanyi.
“Hana lolote huyo, anatapatapa tu. Hakuna cha bosi yeyote anayetembea na mimi, mara anituhumu kuwa namroga, yaani kwa kweli nilifika wakati nikachoka.
“Wakati ndiyo ugomvi unaanzaanza, nilimtumia nauli akaja Kigoma. Alipofika akanigeuka. Kuna wakati aliomba nimtumie picha za utupu, nikampa kama mume wangu, akaanza kuwaonesha watu hadi baba yangu mzazi, muacheni huyo kama alivyo, mimi nimeshamuachia Mungu,” alisema Lilian.

No comments:

Post a Comment