SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UAGIZAJI WA TRANSFOMA ZA UMEME KUTOKA NJE YA NCHI.

Jonas Kamaleki-Maelezo
Serikali imeliagiza Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kutoagiza transfoma nje ya nchi na badala yake kutumia zinazotengenezwa hapa nchini na kampuni ya Tanalec.

Agizo hilo limetolewa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kusini, Mhe. Daimu Iddi Mpakate aliyetaka kujua ni lini Serikali itatoa pesa kukamilisha miradi ya umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Dkt. Kalemani alisema uzalishaji wa transforma ni mkubwa ikilinganishwa na mahitaji ya bidhaa hizo kwa mwezi, hivyo hakuna sababu ya kuagiza transforma hizo kwa bei kubwa wakati zinapatikana hapa nchini.

Kuhusu suala la kugharamia nguzo kwa Mpango wa REA Dkt. Kalemani alisema mteja hatakiwi kutozwa gharama yoyote ziadi ya Tshs. 27,000 fedha ya kuunganishiwa umeme kwa mpango huu.Dkt. Kalemani alisema kuwa Serikali inatekeleza Mradi wa REA Awamu ya II katika Wilaya ya Tunduru na kazi hii inategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016.

No comments:

Post a Comment