HAMIDA HASSAN, WIKIENDA
DAR ES SALAAM: Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ anadaiwa kumtusi staa wa sinema za Kibongo, Wastara Juma baada ya kumuomba msanii wake akarekodie katika studio zake za Wasafi Classic Baby (WCB).
Tukio hilo lililopigwa chabo na chanzo chetu lilijiri wikiendi iliyopita katika moja ya studio za runinga ambapo Wastara alikwenda kumpeleka msanii wake aitwaye Ibrahim Khaan kwa ajili ya mahojiano.
Sosi wetu aliliambia Wikienda kuwa, Diamond alimshushia Wastara matusi kwa madai kuwa ni shabiki wa Ali Kiba na kwamba kwa muda mrefu alikuwa akimsaka ili ampe makavu.
CHANZO CHAFUNGUKA
“Jamani mimi nimemsikia kwa masikio yangu Diamond akimtukana Wastara matusi
ya nguoni, kisa ni ushabiki wake kwa Ali Kiba.
“Unajua Wastara ana msanii wake ambaye ‘anammeneji’, walipokuwa kwenye studio za runinga walikutana na meneja wa Harmonize anayeitwa Momo.
“Huyo Momo anajuana na mdogo wa Wastara hivyo walipoonana walisalimiana kisha akatokea Harmonize ambaye naye alisalimiana na Wastara.
“Wastara ndiye aliyeomba kuonana na Diamond kwa sababu msanii wake alikuwa akihitaji kubadilishana naye mawazo,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, baada ya kuongea na Wastara, Momo alimfuata Diamond kwenye gari akiwa ameongozana na mdogo wa Wastara ambaye alimweleza Diamond kuwa Wastara alikuwa akitaka kuongea naye.
Chanzo kiliendelea kusimulia kuwa Diamond, alianza kutoa maneno mazito na kusema kwa nini asiende kwa Ali Kiba kisha akatukana matusi mazito yasiyoandikika gazetini.
Chanzo hicho kilidai kwamba, wakati Diamond akitoa lugha hiyo kali kwa Wastara, Harmonize alikuwa pembeni hivyo aliinama kwa aibu.
WASTARA NA DIAMOND
Ilisemekana kuwa, Wastara alipomsogelea Diamond alimsalimia Diamond ambaye aliitikia akiwa amekasirika kisha Wastara akaanza kujieleza kuwa alikuwa akihitaji msanii wake akafanyie kazi yake kwenye Studio za Wasafi.
Chanzo kilieleza kuwa Diamond aliendelea kumkejeli Wastara akimhoji kwa nini Wasafi na si kwa Ali Kiba?
Ilielezwa kuwa Wastara alicheka na kumwambia kuwa yeye amependa kurekodia Wasafi na nia yake si ushabiki bali ni kazi tu.
DIAMOND AKATISHA MAONGEZI
Hata hivyo, ilisemekana kwamba, Diamond hakutaka maongezi hivyo alimkatisha kwa kumwambia kuwa jambo hilo amalizane na Momo.
Baada ya habari hiyo kutua kwenye dawati la Wikienda, mwanahabari wetu alimtafuta Wastara kwa njia ya simu ambapo alikiri kukutana na Diamond na kuzungumza naye ishu za msanii wake lakini hakujua kama kulikuwa na matusi.
“Sina ugomvi naye na wala hayo ya matusi sijui ila ni kweli nilikutana naye na nilipanga kwenda kwenye studio yake lakini alinihoji kuhusiana na kuichagua studio yake, nikamweleza natafuta ubora na nitafanyia studio mbalimbali ikiwa ni pamoja na huyo Ali Kiba,” alisema Wastara.
Wikienda lilimtafuta Diamond kwa njia ya simu lakini jitihada za kumpata ziligonga mwamba baada ya kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa hivyo zinaendelea.
No comments:
Post a Comment