Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa kushirikiana na Kampuni ya Udalali ya Yono, wameifungia Kampuni ya Benchmark Productions na kuipa muda wa siku 14, iwe imelipa deni la kodi ya Sh bilioni 7.04, vinginevyo mali za kampuni hiyo zitauzwa kwa mnada.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Meneja Msaidizi wa Madeni wa TRA, Mkoa wa Kinondoni wa Kodi, Sylver Rutagwelera alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuidai kampuni hiyo inayomilikiwa na Rita Paulsen kwa muda mrefu bila kulipa.
TRA, wakiwa na Kampuni ya Udalali ya Yono, walifika eneo la Mikocheni jijini hapo jana asubuhi ziliko ofisi za kampuni hiyo na kuwaeleza wahusika kuhusu deni hilo, na kuwataka waoneshe risiti za malipo iwapo wameshaanza kulipa deni hilo, jambo ambalo wahusika hao hawakuwa nazo.
Hata hivyo Meneja Operesheni wa Kampuni hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Evelyn alifika ofisini hapo na kuwaambia maofisa hao kuwa walishaanza mawasiliano jinsi ya kulipa deni hilo. “Zipo barua tulizokuwa tumeanza kufanya mawasiliano na TRA, kuhusu deni hili, lakini pamoja na hayo, deni lenyewe ni kubwa kuliko uwezo wa kampuni,” alisema Evelyn.

No comments:
Post a Comment