Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary (nyuma) wakiwapungia wananchi baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Dodoma jana, kuanza makazi mapya ya kiutawala.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
TANZANIA leo iliandika historia mpya baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasili uwanja wa ndege wa Dodoma na kudhihirisha wazi kuwa sasa Dodoma ni makao makuu ya nchi na serikali yote itahamia Dodoma.
Alipokewa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama na mamia ya wakazi wa Dodoma.
Ndege iliyombeba Waziri Mkuu iliwasili uwanja wa ndege saa 10.06 alasiri, ambapo alishuka ndani ya ndege akiwa ameongozana na mkewe, Mary, kisha kuwapungia wananchi.
Nje ya uwanja wa ndege, wananchi walijipanga barabarani wakiwa wamesimama na mabango, kama ishara ya kumkaribisha mkoani hapa kiongozi huyo wa juu, ambaye aliahidi Watanzania kuwa angehamia rasmi Dodoma mwezi Septemba.
Miongoni mwa mabango hayo yalisomeka ‘Magufuli Oyee’, ‘Ndege Tumeziona’, ‘Majaliwa Tumemuona’, ‘Tunakukubali’.Mabango mengine yalisomeka ‘Magufuli Tumemkubali, ‘Endelea kutumbua majipu’.
No comments:
Post a Comment