Mkali wa Muziki wa Mduara, Snura Antony Mushi ’Snura’ akiongea na Global TV Online leo.
Snura akiwa katika pozi.
Stori: Denis Mtima/Gpl
BAADA ya kufungiwa na kutakiwa kurekebishwa kwa video ya Wimbo wa Chura ulioimbwa na mkali wa Muziki wa Mduara, Snura Antony Mushi ’Snura’ ambao ulikosa maadili hatimaye video hiyo leo imeruhusiwa kuchezwa.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Snura ambaye pia ni muigizaji amesema kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya Waziri wake, Nape Nnauye imemuandikia barua ya kumruhusu kuchezwa kwa video yake hiyo baada ya kuirudia na kuzingatia vigezo vyote alivyokuwa amepewa awali ikiwemo kuzingatia maadili ya Kitanzania.
Snura aliviomba radhi tena kwa mara nyingine vyombo vya serikali vinavyosimamia sekta ya sanaa kwa kutokufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika uendeshaji wa sanaa nchini.
Amefafanua kuwa anamshukuru, Nape Nnauye kwa kuuruhusu Wimbo wa Chura na video yake kupigwa na kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni baada ya kuona video hiyo ikiwa na ujumbe na maadili ndani yake.
Alifafanua kuwa awali alipewa masharti ya kuwa video yake na wimbo vingefunguliwa pale ambapo angefanya video mpya iliyozingatia maadili ya Kitanzania.
Vilevile alieleza kuwa video hiyo inaeleza maana halisi ya neno Chura kwa kumaanisha ni mwanamke anayerukaruka katika uhusiano wa kimapenzi kwa kubadilisha wanaume mbalimbali na matokeo yake kupata magonjwa hatarishi.
“Nimeona mara nyingi watu waliokuwa kwenye uhusiano linapotokea tatizo baada ya kukaa na kutatua na mwenzake au kutumia familia zao kuwasuluhisha anachukua maamuzi ya hasira kubadili wanaume na kuona ndiyo maamuzi sahihi kwake kumbe anapotea,huyo ndiye Chura niliyemzungumzia mimi kwenye muziki wangu huo.
“Niliamua kumtumia Chura nikiwa na maana ya mdudu anayerukaruka ndiyo maana nikamfananisha na mwanamke asiyetulia kwenye mapenzi na kurukaruka,”alisema Snura.
No comments:
Post a Comment