Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi, Hamadi Masauni akijiandaa kukata utepe kama ishara ya uzinduzi wa kampeni hiyo.
Masauni na Mpinga wakitoa vipeperushi ndani ya moja ya mabasi ya kuelekea mikoani katika stendi ya Ubungo Dar.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani , Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi (DCP), Mohamed Mpinga akiangalia mikanda ya kufunga abiria.
KUELEKEA kipindi cha Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya madereva wameaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali na abiria kutoa taarifa kwa wanaokiuka sheria hizo kwa kutoa taarifa kwa wakati.
Hayo ameyasema leo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi, Hamadi Masauni wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya ‘Paza Sauti’ iliyoratibiwa na Mabalozi wa Usalama Babarani RSA Tanzania katika Kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo Dar.
Akifafanua alisema, kila mtu anawajibu wa kutoa taarifa dhidi ya dereva anayehatarisha maisha katika vyombo vya usafiri.
“Dereva kutokujua sheria za usalama barabarani isiwe kigezo cha kuvunja sheria zilizowekwa kwani waathirika wakubwa wa ajali ni Watanzania ambao ndiyo nguvu kazi ya kesho,”alisema Masauni.
Aidha aliendelea kufafanua kuwa, kampeni hiyo italeta matokeo chanya ambayo yataonyesha kupungua kwa ajali au kutokuwepo kabisa na kufanya Watanzania kuwa salama.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi (DCP), Mohamed Mpinga amesema, kampeni iliyozinduliwa ni jitihada za kikosi cha usalama barabarani katika kupambana na ajali pamoja na kuongeza askari kila sehemu ambayo dereva wamekuwa wakikiuka sheria za usalama barabarani.
Amesema abiria wanatakiwa kuwa chachu ya kutoa taarifa za uvunjifu wa sheria za usalama barabarani kwa madereva ili waweze kuchukuliwa hatua kali.
No comments:
Post a Comment