Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa (Chadema) amekamatwa na polisi leo Jumapili jioni baada ya kushushwa jukwaani kwenye mkutano wa hadhara katika Kata ya Mlandege mkoani Iringa.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema Iringa Mjini (Bavicha), Leonce Marto aliliambia Mwananchi kuwa mbunge huyo alikamatwa saa 11:24 jioni na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) aliyekuwa ameambatana na polisi wengine kisha wakampeleka ofisi za mkoa za jeshi hilo.
“Kutoka Mlandege mpaka ofisini kwa kamanda wa mkoa amebadilishwa kwenye magari matatu. Tunahisi atakuwa anasafirishwa ingawa bado anahojiwa. Yupo ndani, sisi tunaendelea kumsubiri nje,” amesema Marto.
Mwenyekiti huyo alizungumza na Mwananchi kupitia simu ya mbunge huyo na kubainisha kwamba mpaka wakati huo (saa 12:30 jioni) jeshi hilo halikubainisha sababu za kumshikilia Msigwa.
No comments:
Post a Comment