Viongozi wa juu wa Chadema , Freeman Mbowe na Edward Lowassa wataongoza kampeni za uchaguzi mdogo wa nafasi za udiwani kwenye kata 43.
Chama hicho kimeunda Kamati za Kitaifa 10, zitakazoongeza nguvu, hamasa na mikakati ya kampeni za uchaguzi wa marudio kwenye nafasi hizo kuanzia kesho hadi siku ya uchaguzi.
Timu hizo ambazo zitafanya kazi kwa kushirikiana na kamati zingine za hamasa katika ngazi za kanda, mikoa, majimbo, kata na matawi katika maeneo yenye uchaguzi huo, zitaongozwa na Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho Tumaini Makene imeeleza kuwa Mbowe ataanza kuzindua kampeni kesho katika Kata ya Saranga, jijini Dar es Salaam.
Makene ametaja watakaoongoza timu hizo zilizopangwa kwa makundi A hadi G, kuwa ni Mwenyekiti wa Chama Taifa Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, Makamu Mwenyekiti Taifa (Bara), Profesa Abdallah Safari, Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa (Zanzibar) Said Issa Mohamed, Katibu Mkuu wa Chama Dk. Vincent Mashinji.

No comments:
Post a Comment