Wakati katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akiwa nchini Canada kushughulikia suala la ndege ya Bombardier, waziri mkuu wa nchi hiyo, Justin Trudeau amesema hawezi kuingilia uhuru wa mahakama ambayo anaamini itatenda haki.
Hivi karibuni Rais John Magufuli alisema amemwandikia barua waziri huyo mkuu wa Canada ili kujua hatima ya ndege hiyo.
Hata hivyo naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alisema jana kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu waziri mkuu yupo na wao hawajapata taarifa rasmi.
“Lakini kingine naomba utambue kuwa katibu mkuu bado yupo Canada, kwa hiyo mambo mengi mimi sijayapata hadi atakaporudi aje kutu-breaf kilichojiri huko,” alisema Nditiye.
Akizindua uwanja wa ndege mjini Bukoba, Novemba 6, Rais Magufuli alisema amemwandikia barua waziri mkuu wa Canada kumuomba kuachiwa kwa ndege hiyo na amemtuma mwanasheria mkuu wa Serikali, George Masaju kwenda nchini humo kushughulikia suala hilo.
Kwenye barua yake ya majibu ambayo yameripotiwa na gazeti la National Post la nchini humo, waziri mkuu wa Canada Trudeau amesema hana cha kufanya kwa kuwa shauri hilo lipo mahakamani.
No comments:
Post a Comment