Wakati Chadema ikijibu barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuhusu tuhuma za uvunjivu wa sheria ya vyama vya siasa na maadili ya vyama hivyo, huenda chama hicho kikakabiliwa na mambo matatu kama adhabu.
Chadema iliwasilisha majibu ya maelezo kuhusu tuhuma hizo jana katika ofisi ya msajili yakiwa ni ya pili baada ya yaliyowasilishwa awali kutomridhisha msajili.
Awali, Chadema ilitakiwa kutoa maelezo kwa kuvunja sheria kutokana na kufanya maandamano Februari 16 baada ya mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni uliofanyika Mwananyamala kwa Kopa jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuwasilisha majibu hayo wiki iliyopita, msajili alieleza kutoridhishwa na aliiandikia Chadema barua nyingine akitaka maelezo kuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika mkutamo huo wa kampeni alitoa lugha za uchochezi.
Katika barua zote mbili kwa Chadema, Jaji Mutungi amekitaka chama hicho kutoa maelezo ni kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka sheria ya vyama vya siasa na kanuni za maadili ya vyama hiyo.

No comments:
Post a Comment