TUSIPOANGALIA mwisho wa kashfa ya Akaunti ya Dhamana ya Tegeta tutamsikia Rais Jakaya Kikwete akizungumza na kutuambia kuwa alikuwa hajui nini kimetokea na kuwa na yeye, kama sisi wengine, atakuwa ameshangazwa na kushtushwa. Atakapozungumza bila ya shaka atajaribu kutuonesha kuwa jambo hili limemshangaza sana kwani alitarajia baada ya kujiuzulu kwa Edward Lowassa na kuvunjika kwa Baraza la Mawaziri kufuatia kujiuzulu huko alitarajia watendaji wake wangekuwa wamejifunza kitu. Hawakujifunza.
Hata ikitokea mawaziri na Mwanasheria Mkuu pamoja na watajwa wengine kujiuzulu kuna uwezekano Watanzania watajaribu kuaminishwa kuwa kashfa hii inahusu watu wenyewe tu na si serikali na wala isihusishwe na chama. Tayari jaribio hili limeanza kusikika na siku zinavyozidi kuja ndivyo tutalisikia sana bungeni kuhusu wote waliochukua fedha za akaunti ya Tegeta ambayo ilikuwa inashikilia fedha kwa niaba ya Tanesco na IPTL huko Benki Kuu. Tumekwishasikia baadhi ya viongozi wa CCM na wale wa ndani ya serikali wakijitahidi kuwabebesha mizigo watu ambao wanatajwa kukatiwa fedha nyingi na mmojawapo wa wafanyabiashara maarufu nchini, fedha ambazo zinadaiwa ni kutokana na akaunti hiyo ambazo zilichukuliwa baada ya muda mrefu wa migongano ya kisheria kati ya Tanesco, ITPL na kampuni zingine ambazo zilidai kuchukua nafasi ya IPTL. Siyo kusudio langu kuelezea hili sana.
Hata hivyo, hadi hivi sasa hatujasikia kauli yoyote kutoka Ikulu hususan juu ya nafasi ya Rais Kikwete katika suala hili zima hasa kwa vile viongozi wake waandamizi wakiwemo Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi na wengine wametajwa kuwa ni sehemu ya watu waliochukua mgao huo kutoka kwa Rugemalila (mfanyabiashara na ofisa wa mojawapo ya kampuni zilizochukua IPTL). Ni wazi kuwa yawezekana ukimya wa Rais Kikwete kwa sasa unatokana na kuwa yuko anapata nafuu baada ya upasuaji wa tezi dume wiki mbili tu hizi zilizopita.
Uzito wa kashfa hii na jinsi ambavyo inaonekana imegusa watu mbalimbali maarufu nchini na kiasi kinachotajwa kuchotwa na kugawiwa kunalazimisha kujiuliza kama Rais Kikwete alikuwa hajui chochote juu ya jambo hili na kama alikuwa hajui inawezekana vipi na kama alikuwa anajua basi alijua nini na lini? Haya ni maswali muhimu sana kujiuliza kama kweli tunataka kupata kina cha kashfa hii kwani Rais Kikwete inaonekana haiwezekani akatenganishwa na IPTL.
Wakati Horace Kolimba – aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM na Waziri wa Mipango – ameenda Malaysia na akiwa huko kuanza mazungumzo ya kutafuta suluhisho la tatizo la umeme Waziri wa Maji, Nishati na Madini kwa wakati huo alikuwa Jakaya Kikwete. Hiyo ilikuwa Julai 1994. Mwezi Agosti mwaka huo huo ofisa wa juu wa kampuni ya Mechmar, Datuk Majid alifanya ziara nchini na kufanya mazungumzo na Kikwete juu ya jinsi Mechmar ingeweza kusaidia kuondoa tatizo la nishati. Mwezi Septemba makubaliano ya awali (Memorandum of Understanding) yalitiwa saini.
Kwa hiyo tunajua kwa uhakika wa historia kuwa Kikwete anajua kuhusiana na mktaba wa IPTL na licha ya mapingamizi mengi yaliyotolewa na taasisi mbalimbali na nchi wahisani miaka ile ya tisini, CCM na serikali yake waliendelea na mchakato huo. Baadhi ya maofisa ambao walihusika na kuileta IPTL nchini wengi tayari majina yao yanajulikana; Andrew Chenge – aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Abdallah Kigoda ambaye aliingia na kushikilia Wizara ya Nishati na Madini Februari 1997 ni wachache tu kuwataja.
Kwa muda wote ambao Kikwete alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje ndiyo IPTL nayo imekuwa ikishindana na Tanesco na serikali na hivyo uhakika mwingine wa wazi kabisa ni kuwa Kikwete alikuwa na nafasi ya kujua mambo mengi yanayofanyika kutokana na kuwa waziri mwandamizi kwa miaka kumi, muda ambao pia ulitumiwa kutafuta usuluhishi katika mahakama ya kimataifa ya biashara. Hawezi kudai kuwa alikuwa hajui.
Baadhi yetu tunakumbuka kuwa wakati wa kashfa ya rada, Kikwete alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje aliyejitokeza na kutetea ununuzi ule akidai kuwa tulikuwa tunaihitaji licha ya bei ghali na teknolojia ambayo kwa kweli hatukuwa tunaihitaji. Kwenye hili la IPTL ni hivi hivi, karibu watendaji wote waliokuwa wanaipigia debe IPTL inaonekana wazi kabisa walikuwa wanapata makato fulani kutoka kwa wadau wa IPTL. Kuna ripoti nyingi ambazo zilikuwa zinaonesha jinsi James Rumegalila alivyokuwa akisogea karibu na wanasiasa na watu wa karibu wenye kugusa maslahi ya IPTL na kuwalainisha.
Mmojawapo wa watu waliokuwa wamepinga mradi huu tangu mwanzo na labda angeweza kuwa shujaa mkubwa ni Patrick Rutabanzibwa. Ruta – kama wengi walivyozoea kumuita alikuwa amejaribiwa kulainishwa sana na “kakake” Ruge (Rugemalila). Inadaiwa Ruge alishawahi kujaribu kumpa hongo ya dola laki mbili ili abadili msimamo wake wa kupinga ujio wa IPTL; Ruta alikataa na hata zawadi ya X’mass ya shilingi laki tano (mwaka 1994) ambayo Ruge alimwachia nyumbani kwake aliirudisha.
Madai ambayo yametolewa na baadhi ya walioshikishwa hela na Ruge kuwa ni za kirafiki wanawachukulia Watanzania wote kuwa ni watu wasio na kumbukumbu na hili pia inabidi lije kuhoji nia ya kweli ya Rais Kikwete kupambana na ufisadi. Wakati sakata la IPTL linaanza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilishafanya vikao na kukusanya ushahidi mbalimbali ambao ungeweza kusababisha Rugemalila kukamatwa. Inadaiwa Dk. Edward Hosea wakati huo akiwa Mkurugenzi tu ndani ya Idara chini ya Generali Kamazima alitaka kumtia pingu Rugemalila lakini alijikuta anazidiwa na bosi wake pamoja na Mwanasheria Mkuu, Andrew Chenge.
Katika ushahidi mbalimbali uliokusanywa dhidi ya Ruge na ambao bila ya shaka Rais Kikwete atakuwa anaujua kwani Hosea amekuwa mpambanaji wake mkuu dhidi ya rushwa na majina yanaonesha baadhi ya watu mashuhuri na wasio mashuhuri sana wakishikishwa hela ili waunge mkono IPTL. Na ni mtindo ule ule ambao ulitumika miaka ya tisini unaonekana kurudia tena kutumika safari hii kulainisha wanasiasa na watendaji mbalimbali. Miongoni mwa watu waliodaiwa kushikishwa fedha ni: Prosper Victus aliyekuwa ofisa katika Waziri ya Nishati na Madini alipewa ofa na Ruge kuzuia baadhi ya taarifa zisimfikie Rutabanzibwa; huyu anadaiwa kupewa ofa ya dola laki mbili vile vile.
Esther Mzunzu naye alikuwa ofisa chini ya Ruta, yeye anadaiwa kupewa kiasi cha shilingi laki moja.
Lakini zaidi tukumbuke kuwa sakata zima hili halijafichika tangu Kikwete mwenyewe aingie madarakani. Aliingia madarakani tatizo la nishati likiwepo na chini yake tumeshuhudia kashfa za Richmond/Dowans na vile vile hii ya IPTL ikijirudia – ukiondoa kashfa nyingine. Mawasiliano yote ambayo yamepatikana kuhusiana na kesi hii inaonekana bila ya shaka hadi Ikulu walikuwa wanajua kwani kuna barua zimetumwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi – msaidizi mkuu wa Rais na Mkuu wa watumishi wa umma. Kama Katibu Mkuu kiongozi amejua hili dili la kuchukua fedha za escrow ni wazi bila ya shaka hadi Kikwete atakuwa anajua kwani mojawapo ya nakala za barua yenye kuelekeza Benki Kuu kutoa fedha za IPTL ilitumwa kwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Watanzania tutafanya makosa makubwa sana kama tutaangalia kashfa hii na watu wanaohusika kama ni kashfa ya mtu mmoja mmoja tu. Na tutafanya makosa makubwa sana tukidhani kuwa Rais Kikwete hana hatia katika hili. Tutafanya makosa makubwa zaidi kama tutaamini kuwa CCM na serikali siyo wadau katika hili – zipo kumbukumbu za muda mrefu tu za madai ya jinsi CCM yenyewe ilivyoshikishwa fedha ili kuhakikisha IPTL kuingia nchini. Na hata hizi fedha ambazo watu wanafikiria zimechotwa na mtu mmoja mmoja kuna uwezekano mkubwa sana wakati tunaendelea kupiga soga fedha hizi zinazungushwa na kusafishwa (money laundering) hasa tukiangalia baadhi ya watu ambao wanadaiwa kukatiwa mamilioni ya hizo fedha. Akaunti ambazo fedha hizo ziliingizwa tutakapokuja kushtuka hatutakuta akaunti hata moja yenye fedha; tutakuwa tumeliwa na wale wanaosema “Turudishieni Fedha Zetu” itakuwa imekula kwao.
Lakini kwanza, tuanze kumuuliza Kikwete, ulijua nini kuhusiana na uporaji huu na ulijua lini?
- Raia Mwema: Sakata la Escrow: Kikwete alijua na alijua lini?
No comments:
Post a Comment