Mtoto afanyiwa unyama na mama yake mzazi

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa,Jacob Mwaruanda.

Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka sita amefanyiwa visa vya kinyama na mama yake mzazi, ambaye anadaiwa kumjeruhi vibaya kwa kumchoma moto mikono yake na kisha kumfungia ndani kwa siku nne akiugulia majeraha bila kutibiwa wala kula chakula.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, mama aliyefanya ukatili huo (jina linahifadhiwa) ni mkazi wa mtaa wa Eden, Manispaa ya Sumbawanga, mkoani hapa.

Inadaiwa mama huyo alifanya kitendo hicho baada ya kukasirishwa na kitendo cha mwanae huyo kupakua maharage kutoka kwenye chungu na kuyala.
Ilielezwa kuwa mama huyo alikuwa ameyapika maharage hayo kwa ajili ya mlo wa mchana.

Kamanda Mwaruanda alisema mama huyo alikamatwa na polisi Desemba 13, mwaka huu, saa tisa mchana kufuatia taarifa za siri kutoka kwa raia wema kwamba alikuwa akimnyanyasa mwanae huyo ambaye anasoma chekechea mjini hapa .

No comments:

Post a Comment