BARUA YA WAZI KWA KWA RAIS MAGUFULI KUTOKA KWA ALLY SALEH MBUNGE WA JIMBO LA MALINDI, ZANZIBAR


Hon Ally Saleh.

Barua ya Wazi kwa Rais Magufuli. By Hon Ally Saleh. Member of the Union Parliament (Malindi Constituency)
Mheshimiwa
Amiri Jeshi Mkuu
Ikulu, Dar es salaam
Asssalam alaykum,
Natumai hujambo na familia na unaendelea na kazi kama msemo wako wa HAPA KAZI TU ulivyo. Inshallah Mungu atakupa afya na uzima uendelee. Pili nakupongeza kwa kuchagua Baraza la Mawaziri ambalo litafanya kazi na wewe, na sisi kama Wabunge kwa faida ya taifa.
Ingawaje hata hivyo, sikubaliani na wewe juu ya baadhi ya teuzi zako, kama vile kuwanyima fursa ya kutosha Wazanzibari na kuonekana Baraza lako kuwa ni la Tanzania Bara zaidi na kutufanya wadogo zaidi na wanyonge zaidi ndani ya Muungano.
Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, hata hivyo nilotaka kukuandikia leo ni kuhusiana na hali ya usalama hapa kwetu Zanzibar na tishio la kutokuwepo Amani ambapo naamini wasaidizi wako watakuwa wamekuarifu, lakini nakuandikia nikiwa Mbunge wa Malindi kwa tukio lilotokea usiku wa juzi Jumamosi.
Tukio hilo la kuvunjwa vunjwa barza ya wana CUF katika eneo la Michenzani, Mjini Unguja kwa hakika ni muendelezo wa matukio mengi yanayofanywa na watu wanaoitwa wasiojulikana na ambayo yalishamiri sana wakati wa uchaguzi lakini hata baada ya uchaguzi yamekuwa yakiendelea.
Watu waliosemwa wakitumia magari rasmi ya Vikosi vya Zanzibar na wakiwa na silaha walifika eneo hilo usiku mkubwa na kufunga njia na kisha wakifanya ukhabithi huo, na Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu sehemu hiyo ni mita mia tatu tu kutoka Kituo cha Polisi cha Madema.
Tunajiuliza kwa nini tukio hilo lifanywe usiku kama ni zoezi la kawaida la kusafisha mji? Na hilo tunajua kuwa lilitanguliwa na siku chache nyuma gari moja iliyopita na kutangaza kwa bomba kuwa sehemu hiyo ivunjwe, bila ya kuonyeshwa amri halali ya kufanya hivyo.
Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu, sehemu hiyo maarufu huitwa Commonwealth na hadi leo haijaripotiwa kuwa na kitendo chochote kile cha ukosefu wa Amani tokea ilipoanzishwa.
Mita 100 tu upande wa pili kuna ile inayoitwa Maskani Mama ya Kisonge ambayo hiyo haiguswi wala haiulizwi na Polisi yoyote yule. Tokea kuanzishwa kwake hadi leo imekuwa na ubao unaoitwa Sauti ya Kisonge ambao umekuwa na matusi na kejeli kwa viongozi na hasa viongozi wa upinzani.
Ubao huo umekuwa ukichochea fujo, kutoa lugha ya kibaguzi na mara nyingi imekuwa ni chanzo cha kuzusha hamasa za kisiasa hapa Zanzibar, lakini inalindwa utafikiri ni taasisi rasmi ya kiserikali.
Siku chache nyuma, watu wasiojulikana wakiwa na silaha pia walivamia studio ya Hits FM wakati wa usiku na kuichoma moto na kutia hasara kubwa. Lakini hasara kubwa zaidi ni kuzima sauti za watu na kukaba uhuru wa maoni na kujieleza.

No comments:

Post a Comment