HALI tete! Kufuatia Mahakama ya Ardhi, Dar kutengua bomoabomoa ya nyumba 674, bado ripoti inatisha kwa zile nyumba ambazo mahakama haikuzitambua na zile ambazo zilishabomolewa mwishoni mwa mwaka jana.
Moja ya mjengo wa ukibomolewa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wengi waliokimbilia mahakamani, walikuwa wakisukumwa na baadhi ya vigogo wenye mahekalu yao maeneo ya Mbezi, Dar ambao walikuwa wanashindwa kujitokeza mstari wa mbele kwa kuhofia kuhojiwa au kujulikana nyumba zao ambazo walikuwa wakizimiliki kwa siri.
Imebainika kuwa baadhi ya vigogo hao ni wale wanaofanya kazi serikalini ambapo mijengo yao haifanani na mishahara wanayoipata hivyo kuingia kwenye ‘figisufigisu’ ya uhujumu uchumi.
…….Tingatinga likifanya yake.
Wakati hali ikiwa hivyo, imebainika kuwa mfanyabiashara maarufu jijini Dar, Muzamil Katunzi ni miongoni mwa watu ambao wamekumbwa na sekeseke hilo baada ya kubomolewa uzio wa kiwanja chake kilichopo Mbezi Beach.
Naye bosi wa Kampuni ya Udalali ya Majembe Auction Mart aliyejulikana kwa jina moja la Mwamoto, anayemiliki nyumba eneo la Mbezi, yeye ameamua kubomoa mwenyewe sehemu ya ukuta wa nyumba yake kabla ya serikali kuingilia kati ili aweze kunusuru mali zake.
Juzi, kwenye Mahakama ya Ardhi, korti ilisema inatambua nyumba 674 tu zilizopo Wilaya ya Kinondoni, Dar ambazo zina pingamizi la kisheria.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, nyumba ambazo mahakama haikuzitambua, serikali itaamua yenyewe inabomoa lini kulingana na utaratibu wake.
“Sasa hivi tunabomoa maeneo ya Mbuyuni na Hananasif, maeneo mengine kama Mbezi Beach na kwingineko, tunasubiri maelekezo kutoka ngazi za juu,” Arnold Kisiraga, Afisa Utunzaji wa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) aliliambia Amani.
“Wengi wanalia, wengine wamepata presha kwa vile baada ya bomoabomoa hawajui watakwenda wapi,” kilisema chanzo chetu.
Waandishi: Issa Mnally, Boniphace Ngumije, Chande Abdallah na Makongoro Oging’.
No comments:
Post a Comment