Mwandishi wetu
Matukio ya watu kuporwa pesa kisha kuuawa na majambazi yatikisha, bodaboda zadaiwa kuwa tatizoLicha ya shamrashamra za kusherekea kuuona Mwaka Mpya wa 2016, siyo siri kwamba maisha ya Watanzania hayako salama tena, wameanza kuishi kwa hofu kubwa kufuatia matukio ya mauaji ya raia wema ambayo yamekuwa yakifanywa na majambazi nchini kote kwa kutumia pikipiki na watu kuuawa au kujeruhiwa kwa kupigwa risasi.
Utafiti uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba, ndani ya muda wa miezi kumi na mbili au mwaka mmoja wa 2015, watu kadhaa wameuawa na wengine kujeruhiwa vibaya kwa risasi za majambazi ama wakitoka au kuelekea benki.
Moja ya tukio la mauaji lililofanywa na majambazi.
Matukio hayo ya kikatili yamewafanya Watanzania kutoa kilio chao kwa serikali wakisema: “Hakuna aliye salama mahali popote, wakati wowote, jeshi la polisi limeshindwa kutulinda.”
Kauli hizo zimetolewa na watu mbalimbali jijini Dar, kufuatia tukio la hivi karibuni la kuuawa kwa meneja wa oparesheni wa kampuni ya huduma za simu ya mkononi ya Zantel, Gabriel Raphael Kamukala aliyepigwa risasi na majambazi akitokea benki maeneo ya Mikocheni, Dar ambapo alitoka ‘kudroo’ shilingi milioni kumi.
Hata hivyo, tukio hilo lilikuja siku chache baada ya Desemba 14, mwaka huu ambapo watu wanne walijeruhiwa vibaya na majambazi waliokuwa na pikipiki kisha kuporwa shilingi milioni nne, jirani na Baa ya Hongera iliyopo Kijitonyama, Dar wakiwa wanatokea benki.
Kama hiyo haitoshi, Agosti 28, mwaka huu, maeneo ya Jangwani, Dar, mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi waliokuwa na pikipiki aina ya boxer ndani ya daladala iliyokuwa ikifanya safari zake kati ya Mwenge na Kariakoo kisha kupora kiasi kikubwa cha fedha baada ya kumfuatilia mtu huyo kwa muda mrefu.
Miezi michache iliyopita mfanyabiashara mwingine alipigwa risasi na majambazi wenye pikipiki maeneo ya Mtoni-Mtongani jijini Dar, akielekea benki kuweka fedha alizokusanya kwenye kituo cha mafuta.
Matukio mengine ya kutisha katika kipindi hicho cha miezi kumi na mbili ni pamoja na kupigwa risasi kwa mfanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi, Patrick Pera ambaye majambazi walimpora shilingi milioni mbili maeneo ya Tabata Relini, Dar.
Pia lipo tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa kwa risasi kwa walinzi wa Benki ya NMB Tawi la Chanika, Dar lililofanana na lile la walinzi wa Kampuni ya Bonite, Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi huku mwingine akibaki na majeraha makubwa baada ya kuporwa kiasi kikubwa cha fedha na majambazi.
Kabla ya matukio hayo, bado kumbukumbu ya Juni 23, mwaka jana ipo vichwani mwa wakazi wa Dar ambapo sista wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kibangu jijini Dar, Precensia Kapuli (50), aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi eneo la River-Side, Ubungo jijini Dar.
Katika tukio hilo, ilidaiwa kwamba majambazi hao walimfuatilia sista huyo tangu akiwa kwenye moja ya benki zilizopo kwenye Maduka ya Mlimani City alikokuwa amekwenda kuchukua kiasi kikubwa cha fedha ambapo dereva aliyekuwa naye, alijeruhiwa kwa risasi.
Kitendo cha watu kuvamiwa na majambazi wakitokea benki na kuibiwa fedha kisha kuuawa kimeziweka taasisi za fedha katika kashfa kwa watu wengi waliozungumza na gazeti hili wanadaiwa wanatoa taarifa kwa majambazi juu ya mtu kuwa na fedha na mfanyakazi wa benki ambao wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu.
“Hawa wafanyakazi wa benki ndiyo wanaotuuza, wanatoa taarifa zetu kwa majambazi tunauawa,” alidai mmoja wa mashuhuda wa tukio la kuuawa kwa mfanyakazi huyo wa Zantel huku lawama zote zikielekezwa kwa bodaboda aina ya boxer kuwa ni tatizo kwani ndizo zinazotumika katika uporaji kufuatia kuwa na spidi kubwa baada ya kutekeleza uhalifu.
Kwa mujibu wa watu wengine waliozungumza na gazeti hili wamedai jeshi la polisi nchini linashindwa kuwalinda kwani matukio ya ujambazi yamekuwa yakiongezeka tangu mwishoni mwa mwaka jana na hakuna taarifa za kukamatwa kwao na kufikishwa mbele ya sheria kwa majambazi ambao wamekuwa wakikatiza maisha ya watu kila kukicha.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Kamishna Diwani Athumani alisema ni kweli matukio hayo yapo lakini kipo kitengo maalum ambacho kina takwimu kamili ya matukio yote ya ujambazi yaliyotokea mwaka 2015 na namna yanavyodhibitiwa.
“Kwanza huwezi kusema yameongezeka mno kwa sababu ukitazama takwimu za matukio kama hayo utagundua ni machache ukilinganisha na kipindi kingine. Kinachofanyika ni kuyadhibiti yasiendelee kutokea na kuhusu hilo, halina ubishi, Jeshi la Polisi linapambana vya kutosha kuhakikisha watu na mali zao wanakuwa salama,” DCI Diwani Athumani.
No comments:
Post a Comment