Utajiri kigogo NHC gumzo

DSCN4727
Mkurugenzi wa Mikoa na Utawala wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Raymond Mndolwa.
Stori: Waandishi Wetu, UWAZI
DAR ES SALAAM: Baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Mbezi Beach, Kinondoni jijini Dar wameiomba serikali kufuatilia kwa karibu mali za wafanyakazi wao ili kujiridhisha namna walivyozipata kwani utajiri walio nao umekuwa gumzo kwa wengi.
Wananchi hao walizungumza na gazeti hili hivi karibuni wakiwataja vigogo mbalimbali lakini zaidi walimtaja Mkurugenzi wa Mikoa na Utawala wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Raymond Mndolwa (pichani) ambaye walisema mali zake zina gumzo kubwa katika eneo hilo.
“Jamani vigogo wenye mali ni wengi, mimi sitaki kuwaita mafisadi kwa sababu wenye mamlaka ya kutoa jina hilo ni mahakama. “Unaweza kumuita mtu fisadi kumbe mali zake ni halali. Nasema hivi kwa sababu kuna jamaa wa NHC, anaitwa Mndolwa, amejenga hekalu kubwa sana Mtaa wa Ndafu, Mbezi Beach, hebu mfuatilieni, sijajua biashara zake,” kilisema chanzo chetu.
UWAZI LAFIKA MBEZI
Kama ilivyo kawaida ya gazeti hili, lilikwenda Mbezi Beach na kuzipata nyumba mbili za Mndolwa ambapo moja ipo Mtaa wa Ndafu, ina ghorofa moja na ina namba 19, nyingine ina ghorofa nne, ipo Mtaa wa Kidaba na Ndafu. Nyumba hiyo inaendelea kujengwa.
IMG_1427Katika mtaa huohuo wa Mbezi Beach, wakazi wa eneo hilo walisema kuna mahekalu yaliyoibuka hivi karibuni yaliyojengwa na baadhi ya watumishi wa serikali hasa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Shirika la Reli Tanzania (TRL), tena watumishi wengine hawana muda mrefu kazini
BEI YA KIWANJA
“Unajua huku kwetu (Mbezi Beach), bei ya kiwanja tu ni zaidi ya shilingi milioni mia moja ambapo ukimuona mtumishi wa serikali ananunua kiwanja na kujenga mwangalie mara mbilimbili labda kama atakuwa ana miaka mingi kazini na anafanya biashara nyingine,” kilisema chanzo.
Uwazi lilifika kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach, Pantaleo Mushi ambaye kwa upande wake alikiri kuzitambua nyumba zote za Mndolwa lakini hajui jinsi alivyopata fedha za kujengea.
“Labda mtafuteni mwenyewe ili aweze kuwafafanulia jinsi alivyopata fedha lakini kwa upande wangu ni vigumu kujua. Ninachokijua ni kwamba, nyumba ni zake na anafanya kazi NHC ila sijui cheo chake,” alisema mwenyekiti huyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa NHC waliohojiwa na Uwazi kuhusiana na nyumba hizo mbili za Mndolwa, walisema kuwa ni kweli lakini wakasema yupo kazini kwa muda mrefu kwa hiyo kuna uwezekano ni halali lakini walisema mwenyewe ndiye anayejua siri ya kufanikiwa huko.
“Hapa wafanyakazi wengi, hasa vigogo wana mali nyingi ikiwemo majumba, magari na viwanja. Lakini sasa si unajua tena, kupata mali kama hizo inategemea na muda wa kuwa kazini na biashara nyingine. Siyo unaingia leo, mwakani una jumba la kifahari, hilo halikubaliki,” alisema mfanyakazi mmoja.
UWAZI OFISINI KWA MNDOLWA
Ijumaa iliyopita, gazeti hili lilifika kwenye ofisi ya Mndolwa iliyopo maeneo ya Upanga jijini Dar na kufanya naye mahojiano kuhusiana na madai hayo ambapo baada ya kuona picha ya nyumba zake alikiri ni zake huku akisema siyo kosa mtumishi wa serikali kuwa na mali ila inategemea jinsi alivyozipata.
Kigogo huyo alisema nyumba hizo pamoja na mali alizonazo, alizipata kwa kufanya biashara halali na kuongeza kuwa, mali zake zote zipo katika orodha kwenye Ofisi ya Maadili ya Watumishi wa Umma ambao pia wamewahi kufika kwao, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kumfuatilia na kubaini yuko safi.
“Wanaofikiria kuwa nimezipata kwa njia isiyo halali wasiwe na hofu, hizo ni mali zangu na nimezipata kwa njia ya biashara na mkitaka kujua zaidi mnaweza kuniandikia maswali ili niwajibu vizuri kimaandishi (ameandikiwa tayari),” alisema Mndolwa. kwenye Ofi si ya Maadili ya Watumishi wa Umma ambao pia wamewahi kufi ka kwao, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kumfuatilia na kubaini yuko safi .
“Wanaofi kiria kuwa nimezipata kwa njia isiyo halali wasiwe na hofu, hizo ni mali zangu na nimezipata kwa njia ya biashara na mkitaka kujua zaidi mnaweza kuniandikia maswali ili niwajibu vizuri kimaandishi (ameandikiwa tayari),” alisema Mndolwa

No comments:

Post a Comment