Kufungiwa simu; uzembe huu usirudiwe!

simuMUNGU ni mwema kwani katufanya leo tukutane katika safu hii.Leo nitazungumzia mamlaka zinazohusika na kujua ipi ni bidhaa halisi (orijino) au feki baada ya wananchi wengi wasio na hatia kukumbwa na balaa la kufungiwa simu zao na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wiki iliyopita.
Wananchi hao waliokumbwa na balaa hilo wengi wao ni walalahoi, wamepata hasara kubwa ya kupoteza chombo chao cha mawasiliano lakini pia fedha kwa maana ya gharama ya kununua simu hizo ambazo zimetajwa kuwa ni feki.
Nani wa kumlaumu? Wananchi walioletewa simu hizo kutoka nje ya nchi au waletaji au wasimamizi wa bidhaa hizo zinazoingia nchini?
TCRA walikuwa wakiona bila shaka kwenye mitambo yao kuwa simu a ni feki, ikaingia b, baadaye c, d, f kisha zikawa maelfu kwa nini hawakuchukua hatua mapema kudhibiti hadi zikazagaa nchi nzima?
Hii maana yake nini? Ni kwamba wananchi wametapeliwa lakini aliyefanya utapeli huu bila shaka wahusika inawajua na hakuna hatua waliyochukuliwa.
Naandika haya kwa kuwaonea huruma wananchi waliokuwa wakikimbizana na mfumo wa mawasiliano ambao sasa unamlazimisha kila mtu kuwa angalau na simu ya kiganjani kwa sababu ule mtindo wa kuandikiana barua au kutumiana fedha kupitia mabasi sasa umepitwa na wakati.
Nilipata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wasio na uwezo kabisa wa kifedha wa kununua simu mpya wakilalamikia walivyofanyiwa, kuadhibiwa bila kuwa na kosa, wanasema wale walioleta simu hizo na kuingiza nchini waliruhusiwa vipi?
Yupo mwingine alisema bila kigugumizi kuwa kama wao wana makosa kwa kununua simu feki, wamepewa adhabu, vipi wale wanaohakiki uingiaji wa bidhaa hizo feki wamepewa adhabu gani?
Hii si sawa. Vyombo vya dola vinavyohusika na kuhakikisha bidhaa bandia haziingii nchini vifanye kazi vinginevyo wananchi watakuwa wakipata hasara mara kwa mara huku kukiwa na watu waliopewa dhamana ya kuhakikisha bidhaa feki haziingii nchini.
Kuwafungia wananchi walionunua simu feki huku wenyewe wakiwa wanaamini kwamba ni halisi ni kuwaonea. Ni sawa na kumkamata mlaji wa chakula kibovu kilichoingizwa nchini. Huko ni kumuonea kwa sababu inawezekana chakula kile kikawa na madhara mwilini mwake.
TCRA wamesema wamechukua hatua hiyo kwa lengo la kuimarisha usalama kwani simu feki zinaweza kutumiwa katika uhalifu na vyombo vya usalama vikashindwa kumpata muhalifu kwa sababu Imei za simu hizo hazitambuliki kwenye ‘sisitimu’ ya mawasiliano.
Hata hivyo, imechelewa kuchukua hatua hiyo kwa sababu naamini wapo watu waliozitumia simu hizo kufanya uhalifu bila kukamatwa na vyombo vya dola.
Kama ambavyo Rais Dk. John Pombe Magufuli amekuwa akisisitiza, kila mtu sehemu yake ya kazi awajibike, hivyo wote waliohusika na kuachia uingiaji wa simu feki wanapaswa kuwajibika. Cha kusikitisha ni kwamba tunaambiwa kuna bidhaa nyingine nyingi feki nchini. Tuwabebeshe tena mzigo huo wananchi? Hapana, usembe huu usirudiwe.
Nasema hivyo kwa sababu siyo kila kitu mpaka Rais Magufuli aseme, wote tuna nafasi ya kuwakemea wanaozembea kazini.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:

Post a Comment