NI miaka mingi sasa tangu utaratibu wa mabasi ya abiria kusafiri usiku ulipositishwa miaka ile ya mwanzoni mwa tisini. Sababu kubwa iliyotolewa wakati huo ni kudhibiti ajali, kwani madereva walionekana kuzidiwa na usingizi.
Kuanzia wakati huo, iliamriwa mabasi yasafiri mchana na ikifika saa nne usiku, popote yalipo, yasimame ili kusubiri kukuche tayari kuendelea na safari zake. Imekuwa hivyo tangu hapo na inaendelea, hakuna dalili kama kuna mabadiliko yatatokea.
Udhibiti wa ajali hata hivyo, ambayo ndiyo ilikuwa sababu kubwa, haikuonekana kupatiwa dawa, kwani ziliendelea kutokea hata mchana na kuleta madhara makubwa kwa watu na mali zao, kiasi kwamba wakati fulani, ikatolewa amri nyingine ya mabasi yote kufungwa kitu kilichoitwa Speed Governor, ili kudhibiti mwendokasi wa mabasi hayo, jambo ambalo nalo lilifeli.
Katika hali halisi ya mazingira ya Tanzania kwa sasa ni vigumu kutoa sababu moja pekee, kwamba ndiyo inayosababisha ajali za magari, achilia mbali mabasi. Lakini pia, ni vizuri kutazama uwiano wa faida na hasara za kufutwa kwa safari hizi za mabasi nyakati za usiku.
Wakati katazo hili linatolewa, miundombinu ya barabara nyingi ilikuwa mibovu, tofauti kabisa na sasa ambapo karibu miji mikubwa yote imeunganishwa kwa lami. Wakati ule wa zamani, hakukuwa na check points za usalama barabarani, tofauti na sasa ambapo zipo za kutosha kila baada ya umbali kadhaa.
Katika nchi ambayo kasi ya utendaji kazi wa serikali imeongezeka, ikiwa ni pamoja na kuhimiza ulipaji wa kodi, wafanyabiashara wadogo na wa kati, wanaotumia usafiri wa barabara kufanikisha biashara zao ni wadau muhimu wanaopaswa kuangaliwa na utaratibu huu wa kupiga marufuku mabasi kusafiri usiku.
Na siyo wafanyabiashara tu, lakini hata raia wa kawaida, kwa nini wasisafiri usiku ili asubuhi waamke waendelee na kazi? Usafiri wa miji kama Arusha, Moshi, Dodoma, Singida, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Lindi, Mtwara kwenda Dar es Salaam na kinyume chake ni ndani ya saa 12 tu. Kwa nini sheria zisiboreshwe ili mabasi yasafiri usiku?
Kwa mfano, mabasi yawe na madereva wawili kwa ajili ya kupokezana kwa uchovu na usingizi, lakini pia wapimwe kabla ya kuanza safari kama wametumia kilevi na zile check points ziwe imara kukagua mwendokasi.
Tunapotaka Tanzania ya viwanda na kuipa nguvu kauli mbiu ya Rais John Magufuli ya Hapa Kazi Tu, ni lazima pia tufanye kazi kwa saa 24 kwa kadiri inavyowezekana. Dunia yote ndivyo inavyokwenda, mtu asafiri wakati wowote kwa kutumia mabasi.
Kufanya mwisho wa mabasi kusafiri ni saa nne usiku, ni kurudi nyuma wakati tunataka kusonga mbele, kitu cha msingi mamlaka zinazohusika zifanye kazi zao kwa weledi na uaminifu, mchana tufanye kazi Dodoma, usiku tusafiri, asubuhi tuibukie kazini Dar es Salaam!
Nachochea tu!
No comments:
Post a Comment