Uvimbe katika vifuko vya mayai (Ovarian Cyst)

ovariancystdiagram.jpgHII ni hali ya mkusanyiko wa maji kuzunguka kifuko cha mayai. Ni ngozi laini na nyepesi juu ya kifuko cha mayai.
Kifuko cha mayai huwa kinachipua vifuko vidogovidogo Follicles na endapo Follicles hizi zitakuwa na ukubwa zaidi ya sentimeta mbili, basi ndiyo huitwa Ovarian Cyst. Uvimbe unaweza kuwa na ukubwa kuanzia saizi ya punje ya njegere hadi saizi ya ukubwa wa chungwa.
Aina nyingi ya uvimbe huu huwa hauumi na hauwi saratani na huweza kutokea na kupotea ingawa unaweza kuwa mkubwa zaidi. Ovarian Cyst huwatokea wanawake wa umri wote kuanzia watoto wachanga hadi mwanamke anapofikisha umri wa kuzaa.
Baadhi ya aina hizi za uvimbe huleta matatizo mfano kuvuja damu na maumivu makali au kugeuka kuwa kansa.
Endapo uvimbe utakuwa mkubwa zaidi ya sentimeta tano, basi upasuaji utafanyika kuuondoa lakini ukiwa chini ya hapo unaweza kutibika kwa dawa.
AINA ZA UVIMBE WA OVARIAN CYST
Uvimbe huu unaweza kutokea kufuatana na mzunguko wa hedhi na huitwa Functional Cyst ambapo huu wa Ovarian Cyst unaweza kuwa mkubwa endapo utakuwa na zaidi ya sentimeta tano na kuwa mkubwa zaidi hadi kufikia ukubwa hadi usawa wa kitovu.
Uvimbe ambao hutokea wakati wa hedhi kitaalamu huitwa Functional Cyst na umegawanyika kwenye makundi matatu ambayo ni Follicular Cyst, Corpus Luteum Cyst na Thecal Cyst.
Aina hizi za uvimbe huwa hazizidi ukubwa wa sentimeta tatu na wastani hukaa kwa kati ya siku tano hadi tisa na hupotea wenyewe.
Aina hizi zinatokea kufuatana na mfumo wa hedhi uitwao Functional na uvimbe ambao hutokea bila ya uhusiano na hedhi huitwa Non Functional ambao kwa vyovyote huhitaji uchunguzi wa kina.
DALILI
Dalili za uvimbe unaowatokea watoto wadogo wa kike kabla ya kuvunja ungo huitwa Juvenile Ovarian Cyst na umegawanyika katika makundi tofauti. Kama tulivyosema huwa mkubwa hadi kufikia usawa wa kitovu na kumsababishia mtoto alalamike kuumwa na tumbo chini ya kitovu mara kwa mara.
Maumivu haya huwa makali hata kabla uvimbe haujawa mkubwa. Maumivu pia humpata hata mwanamke mwenye uvimbe ambaye tayari ameshakuwa au ameshavunja ungo.
Hapa mwanamke hulalamika maumivu ya mara kwa mara ya tumbo chini ya kitovu na hushika hadi kiuno kwa maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Mtoto mdogo wa kike mwenye uvimbe pamoja na kulalamika maumivu, pia hupata tatizo la kutokwa na mkojo mara kwa mara na kukojoa kitandani, hata kufunga kupata haja kubwa.
Uvimbe huu husababisha mwanamke avurugikiwe na mzunguko wa hedhi, apate maumivu kabla ya hedhi au maumivu makali wakati wa hedhi na damu kutoka kwa muda mrefu na kidogokidogo.
Huhisi tumbo limejaa, zito au hata tumbo kuvimba upande mmoja au lote. Inaweza kutokea uvimbe ukapasuka wenyewe tumboni na kumsababishia maumivu makali sana ya ghafla chini ya kitovu upande wa kulia au kushoto.
Mgonjwa kushindwa kumaliza kutoa mkojo hasa uvimbe unapokuwa mkubwa, yaani ukikojoa mkojo hauishi au unapata haja kubwa haiishi na unajikuta unakaa sana chooni. Mwanamke anayesumbuliwa na uvimbe pia hulalamika maumivu ya kichwa, mwili kuchoka mara mwa mara, kichefuchefu na kutapika pamoja na kuhisi uzito unaongezeka.
UCHUNGUZI
Uchunguzi hufanyika katika hospitali kubwa za rufaa ambapo vipimo vya Ultrasound vitafanyika na ikibidi hata CT- Scan. Kipimo cha damu kuangalia mfumo wa homoni au vichocheo kitafanyika.
TIBA
Matibabu na ushauri matibabu hutolewa baada ya uchunguzi wa kina ambapo utapewa dawa za kutuliza maumivu na nyingine ambazo daktari ataona zinafaa. Uvimbe mkubwa tiba yake inaweza kuwa dawa au upasuaji kutegemea na uvimbe pia kama kuna tatizo la kutopata ujauzito matibabu yatafanyika sambamba na kutibu uvimbe.

No comments:

Post a Comment