Na Richard Bukos na Issa Mnally, UWAZI
DAR ES SALAAM: Jeshi la Polisi Tanzania, linaendelea kushikilia mali za milionea mtoto, Lwitiko Adamson Mwakasala ‘Tiko’ aliyekamatwa Februari 15, mwaka huu kwenye jumba lake la ghorofa lililopo Magomeni Makuti jijini hapa, jirani na Kituo cha Daladala cha Kwa Bi Nyau, kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya ‘unga’.
Utajiri wa Tiko na umri wake, vilianza kuwatia shaka watu wengi kufuatia wingi wa magari ya kifahari, majumba ya kisasa anayomiliki, likiwemo jengo la ghorofa tano analoishi mwenyewe jijini hapa.
Ilikuwa asubuhi ya saa moja ambapo kikosi cha polisi kutoka Kituo cha Oysterbay, Dar kilivamia kwenye nyumba yake ambayo ni ghorofa mbili ikiwa na matawi matatu na kufanya upekuzi mkubwa huku wakitaka kujua chanzo chake cha fedha mpaka kujenga jengo hilo ambalo inasemekana linaweza kuwa hoteli, shule, hospitali au ofisi.
Baada ya kukamatwa, Tiko alishikiliwa kituoni hapo kwa muda na kuachiwa kwa dhamana lakini magari yake hayo yaliendelea kushikiliwa polisi.
Jumamosi iliyopita, Uwazi lilikwenda kituoni hapo kufuatilia kinachoendelea kwenye sakata hilo ambapo liliambiwa milionea huyo alishapelekwa mahakamani baada ya polisi kumaliza uchunguzi wake.
Gazeti hili likiwa kituoni hapo, lilishuhudia magari hayo yakiwa katika muonekano wa kuchakaa na kupoteza mvuto wake kufuatia kupigwa na jua na kunyeshewa mvua.
MAGARI HAYO
Baadhi ya magari hayo yalionekana kuegemea upande mmoja kufuatia kuishiwa upepo kwenye matairi.
Likiwa kituoni hapo, gazeti hili liliwasikia baadhi ya watu wakiyajadili magari hayo huku mwingine akisema yanaozea kituoni hapo.
Mtu mmoja aliyefika kwenye kituo hicho kwa masuala binafsi, alimuonesha mwenzake magari mengine yaliyoozea kituoni hapo na kubaki vyuma chakavu.
Jumla ya magari hayo ni nane, yakiwemo BMW, Toyota Lexus, Land Rover Lumma, Toyota Noah na mengine ambayo, Uwazi halikupata majina yake mara moja.
KAMANDA WA POLISI ANASEMAJE?
Kufuatia hali hiyo, gazeti hili liliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Christopher Fuime ambaye alisema milionea huyo ameshafikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini hapa na yuko nje kwa dhamana.
“Sisi tumeshakamilisha upelelezi wetu na tumeshampeleka mahakamani. Bado tunashikilia mali zake tukisubiri jibu la mahakama. Kama akishinda kesi ndiyo tutamrudishia, akishindwa zinaweza kutaifishwa,” alisema Kamanda Fuime.
Katika tukio la kukamatwa kwake, Uwazi lilifika eneo la tukio na kufanya mahojiano na Mjumbe wa Shina Namba 23, Muharami Daudi ambaye alikuwepo katika zoezi la upekuzi nyumbani kwa Tiko.
Alisema: “Ilikuwa siku ya Jumatatu, saa moja asubuhi, polisi walifika nyumbani kwangu, wakajitambulisha kuwa wametoka Kituo cha Polisi Oysterbay. Wakanitaka nifuatane nao mpaka kwa Lwitiko katika zoezi la upekuzi wa madawa ya kulevya kwamba wana wasiwasi naye katika biashara hiyo.
“Tulikwenda kufanya upekuzi kwa pamoja, lakini hatukupata madawa ya kulevya hivyo polisi waliamua kuondoka na magari yake nane yaliyokuwa pale na bastola kwa uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment