DAR ES SALAAM: Kama ni kweli, huu ni unyama! Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linamshikilia mkazi wa Tabata Mawenzi, Ilinei Nyanja ‘Nei’ (31), ambaye ni fundi ujenzi, kwa tuhuma za kumlawiti mpaka kumuua mtoto Lawrence Mkondya (3), kwenye choo cha jirani.
Chanzo cha habari kilieleza kuwa, Nei anadaiwa kufanya kitendo hicho Agosti 4, mwaka huu kwenye choo hicho baada ya kudaiwa kumkuta mtoto huyo akicheza na wenzake.
Akizungumzia mkasa huo, mama mwenye nyumba aliyokuwa akiishi mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Ashura Miraji, alisema:
“Siku ya tukio, nilimuona marehemu akicheza na wenzake lakini baada ya muda nilimuona akiwa amebebwa na Nei. Sikuwa na shaka naye kwa kuwa Nei ni kawaida yake kucheza na watoto wa rika hilo lakini kuna muda f’lani alitoweka naye.
“Ilipofika kwenye saa moja kasoro usiku, mama wa marehemu, Esther Samson alirudi kutoka kazini na kuanza kumtafuta mwanaye.
“Tulianza kumsaidia kumtafuta wote lakini kuna muda ikabidi tupate wazo la kwenda kuchungulia kwenye choo cha nyumba ya jirani ambacho wenyewe huwa hawakitumii kwa vile wana vyoo vya ndani.
“Kitendo cha kutokitumia choo hicho kwa muda mrefu kimesababisha watu mbalimbali, hasa wahuni kukitumia choo hicho kama gesti bubu.”
Aliendelea kusema: “Ilikuwa ni kama tumebahatisha maana ile kusukuma mlango tu, la haula! Tukamkuta Nei amesimama kama vile mtu aliyekuwa akitusikiliza muda mrefu tulivyokuwa tukihangaika kumsaka mtoto lakini alikuwa akiogopa kutoka.
“Tulimuuliza wewe ndiye uliyekuwa na Lawrence, sasa yuko wapi, mbona hatumuoni? Akajibu alimuacha bondeni kwa mama Happy, amelala.
“Hatukumuamini, ikabidi tuingie chooni humo kukagua. Tulichokiona hatukuamini macho yetu. Tulimkuta mtoto amelala kifudifudi, hajitambui! Amevuliwa kaptula na nguo ya ndani imetupwa ndani ya shimo la choo.
“Kitendo hicho kiliamsha hasira kwa kundi la watu waliokuwa wakimtafuta mtoto ambapo walianza kumpiga makofi na kisha kumpeleka msobemsobe hadi Kituo cha Polisi Tabata ambapo anashikiliwa mpaka sasa.
“Wengine tulimkimbiza mtoto kwenye Zahanati ya Tabata Shule ambapo walituambia mtoto alishaaga dunia kulekule chooni, hivyo tulikwenda Kituo cha Polisi Tabata kwa ajili ya kufanya utaratibu wa kwenda kuhifadhi mwili Hospitali ya Amana ambako walituambia kutokana na kesi yenyewe inabidi mwili huo ukahifadhiwe Hospitali ya Taifa Muhimbili.”
Mama wa mtoto huyo alishindwa kuzungumza na Uwazi kufuatia kupoteza fahamu wakati mapaparazi wetu wakiwa msibani hapo.
Baba wa mtoto huyo, George Mkondya akizungumza na gazeti hili, alisema: “Nasikitika kwa tukio hilo ambalo limenikuta nikiwa safarini kikazi mkoani Mbeya. Tena mwanangu wiki hii ilikuwa ndiyo bethdei yake. Naiomba sheria ifuate mkondo wake ili kukomesha vitendo kama hivi.”
Pia gazeti hili lilizungumza na baba wa mtuhumiwa aliyejitambulisha kwa jina la Jabir Nyanja ambaye alisema: “Siku ya tukio niliporudi nyumbani niliwakuta watu wamejaa, nilipowauliza kulikoni waliniambia mwanangu Nei, amemlawiti mtoto wa jirani mpaka kumuua, sikuwa na cha kufanya zaidi ya kushirikiana na wafiwa katika taratibu zote.”
Akimzungumzia hali ya mwanaye, baba huyo alisema ni mtu mwenye akili timamu na hajui alikumbwa na ibilisi gani.
No comments:
Post a Comment