Uamuzi wa Serikali wa kuzuia daladala zinazofanya safari kati ya Mbezi Louis na Mkoa wa Pwani kutofika Kituo cha Simu 2000 kilichopo Ubungo jijini Dar es Saalam umekuwa mwiba kwa wananchi wa maeneo hayo kutokana na kupaa kwa gharama za usafiri.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa na gazeti hili wamesema tangu Serikali ilipozuia magari kufika katika kituo hicho wanalazimika kuongeza bajeti ya nauli kwa siku kwa wastani wa Sh500 tofauti na ilivyokuwa awali.
Awali, baadhi ya wananchi hao walikuwa wanatumia magari mawili kutoka Chalinze, Mlandizi, Ruvu na Kibaha kuingia jijini hapa, lakini sasa wanalazimika kutumia magari matatu mpaka manne kufanikisha safari zao.
Mkazi wa Kibamba, Erick Adolph amesema kwa sasa anapata shida ya kupata huduma muhimu kutokana na wingi wa abiria anaowakuta Kituo cha Mbezi, huku daladala zikiwa chache. “Ukitokea Kibamba, ukashuka Mbezi unatakiwa kupanda magari ya mwendokasi hadi Kimara, ukifika upande jingine mpaka Posta hapo unajikuta unatumia gharama kubwa inayokaribia Sh2,000 kwa hali ya kawaida watu wa kipato cha chini tunaumia,” alieleza Adolph.
No comments:
Post a Comment