Wasomaji wengi wa safu hii wamekuwa wakiniuliza nini tofauti kati ya kuwa na virusi vya Ukimwi na mtu kuwa na Ukimwi.Ukweli ni kwamba kuna tofauti kati ya mtu mwenye virusi vya Ukimwi na yule ambaye ana Ukimwi, jambo ambalo wengi hawalijui.
Mtu anapokuwa ameambukizwa virusi vya Ukimwi haanzi kuugua mara moja na badala yake huweza kuishi na virusi hivyo kwa muda mrefu hata zaidi ya miaka 10 bila kuonesha dalili zozote.
Tofauti yake na mtu mwenye Ukimwi ni kwamba huyu ambaye anatajwa kuwa anao dalili za magonjwa nyemelezi hujitokeza haraka kutokana na kinga yake ya mwili kupungua kupita kiasi kutokana na kuharibiwa na virusi.
Magonjwa ambayo yatajitokeza ni pamoja na kuharisha, kuvimba tezi mbalimbali mwilini mwake hasa shingoni, kukohoa, kutokwa na malengelenge ya neva za ngozi au kupatwa na mkanda wa jeshi au kuwa na utando mweupe mdomoni.
Hata hivyo, siyo kila anayeumwa maradhi hayo tuliyoyataja hapo juu ni mwathirika wa Ukimwi, hujulikana kuwa ameathirika baada ya kupimwa na kuthibitishwa kwa vipimo.
MTU ANAAMBUKIZWAJE UKIMWI?
Bahati nzuri wengi siku hizi wanajua jinsi Ukimwi unavyoambikizwa. Kuna njia nyingi za mtu kuweza kuambukizwa Ukimwi lakini hapa kuna nne muhimu.
Bahati nzuri wengi siku hizi wanajua jinsi Ukimwi unavyoambikizwa. Kuna njia nyingi za mtu kuweza kuambukizwa Ukimwi lakini hapa kuna nne muhimu.
Virusi vya Ukimwi huishi kwenye majimaji kama vile yale yaliyo sehemu za siri za mwanamke, mbegu za kiume, maziwa ya mama, majimaji ya vidonda, usaha, damu na kadhalika.
Lakini majimaji haya huhitaji njia ya kupita ili maambukizi yatokee. Hivyo basi, mtu anaweza kuambukizwa VVU akiguswa na majimaji ya mwenye Ukimwi kupitia kujaamiiana kwa njia ya kawaida na kinyume cha maumbile au kwa njia ya mdomo (oral sex), hasa kama atakuwa amechubuka sehemu za siri.
Pili, mama mzazi anaweza kumuambukiza mtoto wake Ukimwi wakati akiwa tumboni, wakati wa kujifungua au akiwa anamnyonyesha.
Tatu, mtu anaweza kuambukizwa Ukimwi kwa kupewa damu iliyo na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na nne kwa kuchangia sindano au nyembe ambazo zimetumika na mtu mwenye maambukizo.
Takwimu zilizotolewa na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi zinaonesha kuwa maambukizi kwa njia ya kujamiiana na mtu mwenye maambukizi ni asilimia 82.1. Maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa njia ya kunyonyesha au wakati wa kujifungua ni asilimia 5.9.
Wanaopata maambukizi kutokana na kuongezewa damu yenye virusi vya Ukimwi ni asilimia 0.3 wakati wanaokumbwa na maradhi hayo kwa njia nyingine kama vile kuchangia sindano, nyembe ni asilimia 1.7. na wale ambao wanapata Ukimwi bila kufahamu chanzo ni asilimia 10.
Ni vyema wasomaji wakafahamu njia ambazo haziambukizi kabisa Ukimwi. Mtu hawezi kuambukizwa kwa kuumwa na mbu au kwa kupiga chafya au kukohoa kunakofanywa na mwenye virusi vya Ukimwi.
Mtu hapati maradhi hayo kwa kula, kulala kitanda kimoja, kuogelea bwawa moja, kutumia vikombe au sahani moja kwa chakula au kuchangia choo na mtu mwenye virusi vya Ukimwi.
USHAURI
Mtu aliye na Ukimwi inatakiwa apate mahitaji muhimu ya lishe na jamii ifundishwe kuachana na tabia ya kuwanyanyapaa au kudhani kuwa aliye na Ukimwi ni mzinifu au amekosa maadili.
Mtu aliye na Ukimwi inatakiwa apate mahitaji muhimu ya lishe na jamii ifundishwe kuachana na tabia ya kuwanyanyapaa au kudhani kuwa aliye na Ukimwi ni mzinifu au amekosa maadili.