Kesi ya Mbowe na Vigogo Wengine CHADEMA Yakwama Tena

Kesi ya kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali, inayowakabili viongozi tisa wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kesi hiyo imeshindwa kuendelea leo Julai 18, kwa sababu upande wa mashtaka wanasubiri uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa Mahakama Kuu, na washtakiwa hao.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa ili kusubiri maamuzi ya maombi yaliyopelekwa Mahakama Kuu.

Nchimbi akisaidiana na Wakili Zainabu Mango na Saimon Wankyo, alidai kuwa maombi ya awali yaliyowasilishwa Mahakama Kuu, yalisikilizwa wiki iliyopita na kupangiwa Julai 20, kwa ajili ya kutolewa maamuzi hivyo wanaomba ipangwe tarehe ya karibu kwa ajili ya kusubiri maamuzi yatakayotolewa.

Hata hivyo, wakati kesi hiyo inatajwa jana, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, hakuwepo mahakamani hapo kutokana na kuuguliwa na mke wake ambaye amelazwa katika Hospitali ya Bugando.

"Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa tunasubiri uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa Mahakama Kuu, na washtakiwa hawa," alidai Nchimbi.

Nchimbi baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi Peter Kibatala akisaidia na Jeremiah Mtobesya, alidai kuwa mapingamizi ya awali yameshatolewa, hivyo wanaomba mahakama iendelee kuitaja kesi hiyo.

"Ni kweli John Heche hayupo mahakamani hapa na nimepata taarifa kutoka kwa mdhamini wake, kuwa   anauguliwa na mke  wake, lakini mdhamini wake anazo fomu za matibabu,  ataziwasilisha hapa mahakamani," alisema Kibatala.

No comments:

Post a Comment