Wafungwa jela maisha kwa kusafirisha ‘unga’

By Daniel Mjema, Mwananchi


Moshi. Mahakama Kuu imewahukumu kifungo cha maisha jela, watu wawili baada ya kupatikana na hatia katika kesi mbili tofauti za kusafirisha dawa za kulevya zenye thamani ya Sh289.2 milioni.

Washtakiwa hao waliohukumiwa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Aishiel Sumari ni Hamis Suya, mkazi wa mkoa wa Tanga na Josephine Mumbi Waithera, raia wa Kenya.

Josephine alikuwa akishtakiwa kwa kusafirisha gramu 3,249.82 za dawa hizo aina ya heroini zenye thamani ya Sh146.2 milioni kwenda Vienna, Austria kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia) wakati Suya alikamatwa akisafirisha gramu 3,191.3 za heroini zenye thamani ya Sh143 milioni kwenda jijini Arusha kwa Basi la Happy Nation.

Akitoa hukumu dhidi ya Suya, Jaji Sumari alisema upande wa mashtaka umeithibitishia Mahakama bila kuacha shaka kuwa

alikutwa na dawa hizo.

Alisema hakuna ubishi kuwa tembe 249 za heroini zikiwa ndani ya begi kwenye basi hilo lililokuwa likisafiri kati ya Dar es Salaam na Arusha Novemba 27, 2012 zilikuwa za mshtakiwa huyo.

“Hoja hapa ilikuwa nani ni mmiliki wa begi lile kati ya washtakiwa hawa watatu, yaani Mussa Mgonja, Suya na Abdulaziz Makuka, lakini kulikuwa hakuna ubishi begi la dawa zile lilikutwa ndani ya basi,” alisema Jaji Sumari. Alisema kitendawili hicho kiliteguliwa na maelezo ya Suya aliyoandika polisi na kukiri kosa hilo na kuwa aliyatoa kwa hiari yake bila kulazimishwa.

No comments:

Post a Comment