Hofu ya kutemwa? DC amtishia mwandishi wa habari: "umeamua kutumaliza, tutamalizana…"

3/26/2016 06:16:00 PM
Karen Yunus
Karen Yunus
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Karen Yunus amemtolea maneno ya vitisho mwandishi Neema Emmanuel na kumhoji iwapo kuna mtu anamtuma kutokana na kile alichodai kuwa ni mwandishi huyo kumchafua kwa namna anavyong’ang’ania kuripoti hali mbaya ya Shule ya Msingi Lupemba iliyopo wilayani kwake.

Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2006 na kuwa na wanafunzi 651, ilifungwa kwa muda usiojulikana mapema mwaka huu ili kupisha ujenzi wa vyumba walau vinne vya madarasa. 

Nipashe iliripoti Jumapili iliyopita (Machi 20) kuwa uamuzi wa kuifunga shule hiyo ulitolewa Februari 8, ikiwa ni siku moja tu baada ya gazeti hili kuripoti changamoto mbalimbali zinazokwaza maendeleo ya shule hiyo.

Taarifa ya Nipashe ilikua siku mbili tu baada ya Rais John Magufuli kueleza katika maadhimisho ya kilele cha miaka 39 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Singida kuwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa mikoa watakosa sifa katika serikali yake ikiwa kwenye maeneo yao kutakuwa na wanafunzi wanaoketi chini kwa kukosa madawati.

Aidha, Nipashe ilieleza katika habari hiyo ya Jumapili iliyopita (Wanafunzi wachunga ng’ombe Magu wakisubiri madarasa kujengwa), kuwa baada ya kufungwa kwa shule ya Lupemba huku wanaoendelea na masomo wakiwa ni wanafunzi wa madarasa ya nne na saba peke yake, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijihusisha na shughuli nyingine zisizokuwa za masomo nyumbani kwao ikiwa ni pamoja na kuchunga ng’ombe.

Baada ya kuchapishwa kwa habari hiyo, DC Karen alimpigia simu mwandishi na kumpa vitisho kutokana na kile alichodai kuwa hajamtendea haki. DC Karen alipiga simu hiyo Jumapili iliyopita, majira ya subuhi.

“Haya mambo unayoyafanya siyo mazuri kwa sababu tunajitahidi… lakini wewe unaendelea kutuchafua tu, hujatenda haki,” alisema DC Karen katika moja ya matamshi yake kwa mwa mwandishi na kuongeza: 

“…kwa sabababu haya mambo unayoyaandika yanasomwa na wengine ambao wana maamuzi makubwa… wee unatumwa nini? Kuna mtu anakutuma? Na kama hakuna mtu anakutuma kwa nini unang’ang’ania hivyo?”

Aidha, katika vitisho vyake hivyo kwa mwandishi, DC Karen aliyehamishiwa Wilaya ya Magu akitokea Sengerema kutokana na mabadiliko aliyoyafanya Rais Jakaya Kikwete Februari mwaka jana, alimuonya mwandishi kwa kumuelezea kuwa ni mtoto mdogo anayelingana na mtoto wake wa mwisho na kwamba, kitendo chake cha kuripoti suala la Shule ya Lupemba bila ‘kubalance’ ni sawa na kutaka kuwamaliza na hivyo ajue kuwa "tutamalizana".

“Mi nakwambia... halafu wee bado mtoto mdogo… wee una miaka mingapi… wewe ni mwanangu wa mwisho… mi nakwambia Neema… lakini kwa sababu umeamua kutumaliza, tutamalizana… lakini na wewe you should wait for your chance (usuburi nafai yako), na hayo mambo yapo nakwambia," alisema DC Karen katika baadhi ya vitisho alivyotoa kwa mwandishi.

"Andika neno karma… usipende kuharibia watu wanajihangaikia maisha yao, kwa miaka mingi, eeh.”

Kwa mujibu wa kamusi ya Kiingereza ya Oxford, neno ‘karma’ lina asili ya Kibudha na Kihindi na maana yake ni malipo anayoweza kuyapata mtu kutokana na matendo yake; kwamba akitenda ubaya hulipwa ubaya na akitenda mema atalipwa kwa wema wake.

UKWELI KUHUSU SHULE YA LUPEMBA

Nipashe imekuwa ikiripoti mfululizo wa taarifa kuhusiana na ukosefu wa miundombinu na changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo ya Lupemba yenye wanafunzi 651, na ambayo ilijengwa mwaka 2006.

Kwa mara ya kwanza, Nipashe iliripoti taarifa hiyo Jumapili ya Februari 7, 2016 huku ikiwa na kichwa cha habari ‘Elimu ya bure mtihani mzito’, pamoja na picha ya ukurasa wa mbele inayoonyesha baadhi ya wanafunzi wakiwa wamekalia vitofali katika mojawapo ya banda la miti na nyasi lililokuwa likitumiwa kama darasa. 

Wiki iliyopita, Nipashe iliripoti tena juu ya shule hiyo, kwa kueleza athari zitokanazo na uamuzi wa Feberuari 8, wa uongozi wa wilaya ambao ni kuifunga kwa muda usiojulikana ili kupisha ujenzi wa vyumba vya madarasa walau vinne na kwa ujumla kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu shuleni hapo. 

Aidha, katika taarifa hiyo, zilioenekana picha za wanafunzi wa shule ya Lupemba wanaolazimika kusaidia wazazi wao shughuli za kila siku ikiwamo kuchunga ng’ombe baada ya shule yao kufungwa kwa muda usiojulikana.

Katika tarifa hiyo, mwandishi alikutana na wanafunzi kadhaa na kuzungumza nao ambapo walielzea masikitiko kutokana na uamuzi wa kufungwa kwa shule yao na wao kurudishwa nyumbani badala ya kuhamishiwa walau kwa muda katika shule nyingine.

Aidha, mwandishi alizungumza pia na wazazi wakiwamo Mathias Musuka na Salome Makoye, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Lupemba, Daniel Matemi; mwalimu wa kawaida, Johannes Rutaihwa; Kaimu Afisa Elimu ya Msingi wilayani Magu, Veronica Justine; Mkurugenzi Msaidizi wa Udhibiti wa Ubora wa Shule Wilaya ya Magu, Joseph Kaswa; Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Ntinika Paul ; aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo na pia yeye mwenyewe, Mkuu wa Wilaya ya Magu - Karen Yunus.

“Ni kweli nimepata vitisho kutoka kwa Mkuu wa Wilaya… lakini sioni nilichokosea kwa sababu hakuna lisilokuwa la kweli katika ripoti hiyo,” alisema mwandishi Neema wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii kuelezea vitisho alivyopata kuhusiana na ripoti juu ya hali ya shule ya msingi Lupemba. 

"Shule imefungwa na wanaosoma ni madarasa ya nne na saba, kuna watoto hivi sasa huishia kuchunga ng’ombe. Yote hayo ni kweli tupu."

Je, hivi sasa hali katika shule hiyo ya Lupemba ikoje? Usikose kufuatilia mwenendo wa ripoti maalum kuhusu shule hiyo katika gazeti hili kesho).

No comments:

Post a Comment