Magufuli afyeka mishahara ya vigogo



Rais John Magufuli 
By Rehema Matowo, Mwananchi rmatowo@mwananchi.co.tz

Chato. Rais John Magufuli ametangaza kiama cha watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma waliojipangia mishahara minono kufikia Sh40 milioni akiahidi kuifyeka hadi kiwango kisichozidi Sh15 milioni kuanzia bajeti ijayo ya fedha ikiwa ni punguzo la asilimia 63.

“Atakayeona kiwango hicho ni kidogo namshauri aanze kutafuta kazi sehemu nyingine kwa sababu hatuwezi kuendelea kulipana mishahara minono kiasi hicho katikati ya wananchi wanaoishi katika lindi la umaskini,” alisema Rais Magufuli na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mazaina mjini Chato jana katika siku yake ya kwanza nyumbani kwake tangu achaguliwe kushika wadhifa huo, Rais Magufuli aliahidi kupandisha mishahara ya watumishi wa chini ili kupunguza tofauti ya kipato kati yao na wale wa juu. “Katika Serikali ninayoongoza, sitegemei kumlipa mtumishi zaidi ya Sh15 milioni; tayari nimeunda tume kushughulikia suala hilo,” alisema na kuongeza: “Kiwango tunachopunguza kutoka kwenye mishahara minono ya wakubwa tutawaongezea watumishi wa chini ambao baadhi wanalipwa mishahara midogo inayoanzia Sh300, 000.

No comments:

Post a Comment