Mwezi huu wa tano tayari kuna matukio zaidi ya matano ya mauaji ya kikatili ya watu kuchinjwa au kukatwakatwa kwa mapanga.
Linaloshangaza wengi na kuibua maswali ni staili ya wauaji ya kuua bila kuchukua kitu chochote kutoka kwa wanaouawa jambo linalotia shaka kwamba huenda wauaji siyo majambazi.
Tukio la hivi karibuni ni la kuuawa kwa Aneth Msuya (30), aliyeuawa kwa kuchinjwa usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita Kigamboni jijini Dar es Salaam kisha waliofanya unyama huo wa kikatili kudaiwa kuondoka na televisheni.
Kama hilo halitosjhi, usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita, watu wawili mume Saidi Somba (48) na mkewe Kadogo Ehicho (47), waliuawa kikatili katika Kijiji cha Mmazani wilayani Butiama, mkoani Mara kwa kukatwa na mapanga wakiwa kwenye nyumba yao.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mmazami, Jackson Kitukuru“, waliotenda unyama huo walichukua simu ya mkononi aina ya Tecno na wakatokomea kusikojulikana.
Mei 19,mwaka huu watu 15 wakiwa wameficha nyuso zao walivamia msikiti katika Mtaa wa Utemini wilayani Nyamagana, Mwanza na kuwaua watu watatu waliokuwa wakiswali usiku kwa kuwakatakata mapanga na shoka.
Mashuhuda walisema kwamba wauaji hao walidai hatua hiyo ilitokana na kitendo cha waliouawa kuswali wakati wenzao wanashikiliwa na polisi.
Mwezi huuhuu, watoto wanne wa familia moja inayoishi Kijiji cha Msufini, Kata ya Ndungu wilayani Same, Kilimanjaro waliuawa kwa kukatwakatwa mapanga wakiwa wamelala baada ya kuvamiwa na mtu aliyedaiwa kuwa ni ndugu yao na baba wa watoto hao akasema kwamba hajafahamu sababu ya kufanya ukatili huo kwani hawakuwa na ugomvi naye.
Tukio lingine lililotokea mwezi huu ni lile la watu saba wa familia moja kuuawa wilayani Sengerema mkoani Mwanza, nao waliuawa kwa kukatwakatwa na mapanga na watu wasiojulikana.
Lakini pia wiki iliyopita askari wa usalama barabarani, Ally Kinyogoli aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake.
Hakika matukio hayo yanatishia usalama wa raia na mbaya zaidi hatujasikia kauli ya serikali ya kulaani mauaji haya ambayo yamekithiri na kuwatia hofu wananchi kwani wanaouawa ni watu ambao hawana hatia.
Mimi nilitegemea wizara ya mambo ya ndani ingetoa kauli kupitia Bunge linaloendelea sasa katika jengo lake mjini Dodoma.
Kwa kweli ukimya huu wa serikali unawafanya wananchi kila mmoja kuwa na mawazo yake kichwani na tayari wengi wanaweza kufikiria njia mbadala za kujihami jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa nchi.
Nashauri serikali kupitia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni itoe tamko bungeni sasa ili hali hii isizidi kuwapa hofu wananchi.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
No comments:
Post a Comment