Maelekezo ya Zitto Kabwe Kwa Wanachama wa ACT- Wazalendo Kuhusu Kauli ya Rais Magufuli Jana Singida

SeeBait

Maelekezo ya Kiongozi wa Chama ( KC ) kwa wanachama wote wa ACT Wazalendo ( KC/01/2016 ).

Tangu kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 Utawala mpya umekuwa ukifanya kila juhudi kuminya uwezo wa Vyama vya Siasa kufanya Kazi zake kwa kisingizio kuwa huu ni wakati wa kufanya Kazi na kwamba Siasa zisubiri mwaka 2020. 

Chama chetu kilipinga kwa nguvu zote uzuiaji huu wa shughuli za kisiasa kwani ni kinyume cha Katiba ya Nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa, sheria namba 5 ya mwaka 1992 kama ilivyofanyiwa marekebisho Mara kwa Mara.

Mnamo tarehe 5 Juni 2016 Chama chetu kilifanya Mkutano wa Hadhara Mbagala jijini Dar Es Salaam na kutangaza Operesheni Linda Demokrasia. Lengo la Operesheni hiyo ( Tamko la Mbagala 2016 ) ni kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa Nchi ya kidemokrasia na kuepuka mwelekeo wa Utawala wa Imla ambao ni utawala wa kidikteta. Chama chetu asili ya uundwaji wake ni kupinga tabia za kidikteta tulizokumbana nazo ndani ya Vyama tulivyokuwamo. 

Hivyo ilibidi tuwe mstari wa mbele kupinga dalili zozote za kuielekeza Nchi kwenye Uimla. Vyama unaweza kuunda utakapo, Nchi huwezi kuiunda ndio maana ni LAZIMA Sisi Kama wanachama wa Chama cha Wazalendo kupinga kwa nguvu zote kuminywa kwa Demokrasia na kuilinda kwa nguvu zetu zote.

Kufuatia Tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano kwamba shughuli za kisiasa zimezuiwa kwa niaba yenu nilitaka Vyama vyote vya Siasa nchini na wadau wengine wa demokrasia kuungana kwa pamoja kukataa Tamko hili ambalo linavunja Katiba ya Nchi ambayo Rais ameapa kuilinda na kuitetea. Wito wetu unanukuliwa hapa chini;

"Tunatoa wito kwa Vyama vyote vya siasa nchini kuunganisha nguvu katika kuhakikisha tunapigana vita [ dhidi ya udikteta] pamoja. Huu ni wakati wa vyama vya siasa na wanasiasa kuacha tofauti zao na kupambana kulinda uhuru wa kufanya siasa wakati wowote kwa mujibu wa Sheria."

Hata hivyo, hakuna Kiongozi wa Chama chochote kile ambaye aliona umuhimu wa kuunganisha nguvu na hivyo kujikuta kila Chama kinaendelea na operesheni zake. 

Viongozi wetu akiwemo Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu walifanya juhudi zote kuwasiliana na watendaji wenzao wa Vyama vingine ili kufanya Kazi pamoja japo kwa uratibu lakini hatukupiga hatua yeyote ile.

Hivyo, Sisi sio sehemu ya operesheni yeyote ile iliyotangazwa na Chama kingine chochote kile isipokuwa Operesheni Linda Demokrasia ambayo sasa itaitwa Tamko la Mbagala la Juni 5, 2016.

Akiwa ziarani mkoani Singida, Rais amefafanua agizo lake la kuzuia mikutano ya kisiasa. Rais amesema kwamba hajazuia wabunge na madiwani kufanya mikutano ' KWENYE MAJIMBO YAO'. Kwanza Rais hana mamlaka ya kuruhusu au kuzuia Kazi za Wabunge na madiwani. Haya ni mamlaka ya KATIBA na sheria za Nchi. Hivyo ufafanuzi wake hauna maana yeyote ile.

Jambo la kushtusha ni agizo la Rais kwamba Wabunge hawana mamlaka ya kufanya mikutano nje ya majimbo yao. Hii ina maana hata Viongozi wa kisiasa ambao sio wabunge hawataruhusiwa kufanya mikutano ya kisiasa. Hii HAIKUBALIKI. 

Anna Elisha Mghwira ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, anazuiwaje kufanya mikutano na wanachama wake nchini? Anazuiwaje kuongeza wanachama? Lakini mama Anna Mghwira aligombea Urais, kwanini asifanye mikutano kuwashukuru waliompa Kura japo hazikutosha?

Uchambuzi wa kitaalamu
Ni dhahiri Serikali ya Awamu ya Tano na sasa Chama tawala wameamua kubadili mwelekeo wa Nchi kisiasa ( kwa kubana uhuru wa kidemokrasia ) na kiuchumi ( kwa kuelekeza nguvu kwenye uchumi unaoelekezwa/endeshwa na dola ). Udhibiti wa Vyama vya Siasa ni moja ya hatua ya udhibiti wa jamii kwa ujumla wake. 

Siku za usoni tutaona udhibiti wa waziwazi wa vyombo vya habari na kwa sasa tunaona namna Asasi za Kiraia ( CSOs) zilivyo kimya tofauti na miaka michache ya nyuma. Hizi zimejiweka kimya zenyewe na zitakazoinua sauti zitafuatiliwa na dola. Yote haya yanaturudisha nyuma katika katika kujenga Tanzania ya Kidemokrasia na yenye Maendeleo.

Utawala wowote ' regime ' hutaka kupata nguvu ya wananchi katika kujijengea uhalali. Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuichukua vita dhidi ya ufisadi kama njia ya kujijengea uhalali na kwa kweli wananchi wengi waliochukizwa na vitendo vya kifisadi wanaunga mkono juhudi hizo. 

Katika ziara yake ya Singida, Rais amenza kutumia maneno kama ' mabeberu ' na ' Maadili ya Mwalimu Nyerere ' maneno ambayo hayajawahi kutamkwa na kinywa chake. Hii inaonyesha kuwa Rais anaanza kukua/kukuzwa kiitikadi na hii itampa uhalali zaidi mbele ya jamii. 

Hata Uamuzi wake wa kutekeleza maamuzi ya kuhamia Dodoma, na iwapo atatekeleza, itamjengea zaidi uhalali. Rais atautumia uhalali huu kujikita katika utawala na kuminya zaidi Demokrasia.

Maelekezo ya Kiongozi wa Chama ( KC )
1. Chama cha ACT Wazalendo kiliundwa kwa madhumuni ya kurejesha Nchi kwenye misingi. Kupitia Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha tumeeleza misingi hiyo kwa kina. Naelekeza kwamba wanachama wote wa ACT Wazalendo wasome, kuelewa na kujadili Azimio la Tabora na kuchambua muktadha wake katika mazingira ya sasa ya Siasa za Nchi yetu.
 
2. Kila Mwanachama wa ACT Wazalendo asione aibu kuunga mkono maamuzi yeyote ya Serikali au Chama kingine cha Siasa yanayoendana na Azimio la Tabora hususan vita dhidi ya ufisadi na kurejeshwa kwa Miiko ya Uongozi.
 
3. Kila Mwanachama wa ACT Wazalendo akatae kwa namna anayoweza lakini kwa Amani mbinu zozote za kuminya Demokrasia nchini. Tamko la Mbagala la kulinda Demokrasia litumike kuongoza juhudi hizo. Chama chetu hakijatangaza maandamano na hivyo wanachama wetu wasiingie katika mambo hayo. 

Hata hivyo kila mwanachama wa Chama chetu aandike barua kwa Rais Magufuli kwa namna anavyoona yeye kumtaka aache kuingiza Nchi kwenye utawala wa Imla. Chama chetu kina wanachama 431,120 wenye kadi. Ikulu ikipata barua 200,000 kutoka kila kona ya Nchi itafunguka macho.

Mwisho
Nawataka wanachama wa Chama Cha ACT Wazalendo kukumbuka kuwa uasili wa Chama chetu ni kupinga kuburuzwa, ufisadi na Siasa za ujanja ujanja. Tujitahidi kwa nguvu zetu zote kutofanya yale ambayo Sisi tumeyakataa.

Viongozi wa kuchaguliwa kwenye vyombo vya uwakilishi Kama madiwani na wabunge wawe makini sana kutii Chama na misingi ya chama. 

Tuwe mstari wa mbele kupinga ufisadi kwani rushwa ni adui wa Haki. Tuwe mstari wa mbele kutaka kurejeshwa kwa Miiko ya Uongozi. Sisi ndio Chama pekee chenye itikadi iliyo wazi. Tusiammie itikadi yetu popote tulipo na bila woga wala aibu.

Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama
30/7/2016

No comments:

Post a Comment