Mkurugenzi Bagamoyo atumbuliwa mapema



Azimina Mbilinyi
RAIS John Magufuli, ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Azimina Mbilinyi.
Taarifa ya Ikulu iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Musa Iyombe, imesema kuwa Rais hajaridhishwa na utendaji wake.
Ingawa taarifa hiyo haikufafanua zaidi, lakini wakati wakurugenzi hao walipokuwa wakila Kiapo cha Uadilifu wa Uongozi wa Umma katikati ya mwezi huu, Rais Magufuli alisema kila mkurugenzi aliyechaguliwa, atambue kuwa sifa zake zilichambuliwa na Rais mwenyewe.

Hata hivyo, aliwataka kuhakikisha wanasimamia vyema fedha za serikali zinazowasilishwa katika halmashauri na kuepuka kuburuzwa, kujipendekeza, kukejeliwa au kutumika vibaya kwa kuingia mikataba na kampuni feki zisizoweza kutekeleza vyema wajibu wake.
Magufuli alisema anazo taarifa za baadhi ya wakurugenzi, walikuwa wakishirikiana na mameya, madiwani na wenyeviti wa halmashauri kwa kupitisha na kuingia mikataba na kampuni zilizo na uwezo chini ya viwango katika kutekeleza miradi ya barabara na matokeo yake miradi mingi haikuwa na mafanikio.
Aliwaasa kuwa wakisimamia maadili hakuna atakayewafukuza kazi na kuwataka wasijipendekeze kwa mtu kwa sababu hakuna aliyepenyeza majina yao kwake hadi wakateuliwa. Aliwataka kuwa makini na kusimamia vyema Sh bilioni 18.77 zinazotolewa na serikali kila mwezi kwa ajili ya elimu bure katika shule.

No comments:

Post a Comment