UPANDE wa Jamhuri umeiomba Mahakama itupilie mbali kiapo kinachounga mkono maombi ya dhamana ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu na wenzake kwa kuwa kina mapungufu ya kisheria.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Shedrack Kimaro akisaidiwa na Theophil Mutakyawa alitoa ombi hilo jana mbele ya Jaji Eliezer Feleshi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati akiwasilisha hoja za pingamizi la awali.
Kesi hiyo ilitajwa jana, lakini kabla ya kuanza kusikilizwa kwa maombi hayo, Kimaro alidai wamewasilisha pingamizi kwa kuwa, kiapo hicho kina mapungufu.
Akielezea mapungufu hayo, Kimaro alidai katika aya ya tatu, Wakili Michael Ngalo aliyeapa kwa niaba ya wakili mwenzake Semi Malimi anaeleza anamwakilisha mleta maombi wa kwanza (Maimu) peke yake pia ameapa kuwa maelezo yaliyopo kwenye kiapo hicho ni kwa mujibu wa uelewa wake mwenyewe.
Alidai kutokana na hilo kiapo hicho hakistahili kuwawakilisha waleta maombi wote na kama kingekuwa kinawahusu wote basi kuna vitu ambavyo wakili aliyeapa alitakiwa avieleze katika hati hiyo iliyowasilishwa mahakamani.
Aidha, aliongeza kuwa, pamoja na wakili ayeapa kueleza anamuwakilisha mleta maombi wa kwanza lakini katika aya nyingine, anaeleza mambo yanayowahusu waleta maombi wote pamoja na matukio ambayo yalitokea kabla hawajafikishwa mahakamani.
Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na Wakili Ngalo akidai kuwa hoja za serikali hazina mashiko, kwani vipengele vilivyo na upungufu haviathiri kiapo, pia hawajaeleza watapata athari gani kutokana na mapungufu hayo.
Aidha, alidai maombi yaliyopo mahakamani hapo, yamefuata taratibu zote za kisheria na kama Mahakama itaona kuna mapungufu hayo, bado ina uwezo wa kuyaondoa, badala ya kukiondoa kiapo chote.
“Mapungufu yaliyopo kwenye kiapo ni madogo, yanaweza kufutwa bila kuathiri lolote katika kiapo, hivyo tunaomba Mahakama ione hoja za pingamizi hazina mashiko,” alidai.
Mbali na Maimu, washtakiwa wengine waliowasilisha maombi ya dhamana ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa Nida, Benjamin Mwakatumbula, Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji wa Nida, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.
Washtakiwa hao na wenzao Meneja Biashara wa mamlaka hiyo, Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Joseph Makani ambao wapo nje kwa dhamana, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 1.2.
|
No comments:
Post a Comment