Watoto wa mitaani Dodoma kuondolewa


SERIKALI mkoani Dodoma itafanya operesheni ya kuwaondoa watoto wa mitaani, ambao wamekuwa kero kwa wapita njia na wateja wanaokula hotelini, ambao huwanyang’anya chakula na hata vinywaji wateja.
Akizungumza na gazeti hili leo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christine Mndeme alisema watawaondoa watoto hao kutokana na kuwa hatari kwa maisha ya watu wengine. Mndeme alisema watoto hao wamekuwa wakikaa makundi na kuvuta dawa za kulevya aina ya gundi na wamekuwa wakiingia kwenye hoteli na kunyang’anya wateja vyakula na hata vinywaji.

“Idara ya Maendeleo ya Jamii itaanza kuwaondoa watoto wa mitaani wanaovuta bangi na petroli,” alisema.
Alisema watoto hao wamekuwa wakikaa kwenye makundi na kuwa tishio kwa wapita njia hasa nyakati za jioni kutokana na kujihusisha na uhalifu.
Pia alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watoto hao kuingia hotelini na kuwanyang’anya wateja chakula na vinywaji kisha kukimbia, jambo ambalo halileti picha nzuri na vitendo hivyo vinatakiwa kudhibitiwa.
“Tutazitambua familia wanakotoka watoto hao, watarudishwa walikotoka na wengine watapelekwa shuleni,” alisema Mndeme.
Alisema wanachukua hatua hiyo kwa umakini ili watoto watakaoondolewa wasirudi tena mitaani, kwani inaonesha miaka ya nyuma lilifanyika lakini baada ya muda watoto hao walirudi tena mitaani.

No comments:

Post a Comment