JINSI KERO MAJI INAVYOWATESA WANAWAKE KISHAPU- SHINYANGA



Mkazi wa kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu akichota maji ya kunywa baada ya kufukua mchanga pembezoni mwa mto Tungu unaotenganisha wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu na Kishapu mkoa wa Shinyanga,mto huo ni tegemeo kubwa la wananchi wa wilaya ya Kishapu kutokana na uhaba wa maji.

Wakati nchi ya Tanzania ikiadhimisha wiki ya maji,imeelezwa kuwa wanawake wengi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji hivyo kushindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo kikamilifu.
Wanawake hao wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutafuta maji katika mto Tungu unaotenganisha wilaya ya Kishapu na Maswa mkoa wa Simiyu kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika mpaka sasa hali inayowafanya kuendelea kuwa tegemezi kwa wanaume.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea wilayani humo wananchi wa vijiji vya Nyenze na Ng’wang’holo kata ya Mwadui Lohumbo wilayani humo walisema maji ni changamoto kubwa inayorudisha nyuma maendeleo ya wananchi kwani wanatumia muda mwingi kutafuta maji.
Walisema licha ya kuishi karibu na mgodi wa almasi wa Williamson wanalazimika kutembea umbali takribani kilomita tano kufuata maji katika mto Tungu unaotenganisha wilaya ya Kishapu na wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.
Akielezea changamoto hiyo,mkazi wa kijiji cha Nyenze Agnes Daudi alisema akina mama ndiyo waathirika wakubwa kwani wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutafuta maji na mara nyingi huamka kila siku majira ya saa 11 alfajiri kwenda katika mto huo na kurudi nyumbani saa 4 asubuhi.
“Licha ya kutumia muda mwingi kufuata maji,hayo maji yenyewe ya mto Tungu siyo salama kwani yanatumiwa pia na wanyama kama fisi na watu wengi kijijini huwa hawachemshi maji wanakunywa hivyo hivyo”,alieleza Daudi.

No comments:

Post a Comment