Na WAANDISHI WETU
-KIBITI, DAR ES SALAAM
TUKIO la kuuawa kwa askari wanane waliokuwa wakitoka doria katika Kijiji cha Jaribu wilayani Kibiti, lina kila dalili kutekelezwa na watu wenye ujuzi na malengo mapana.
Tukio la sasa ambalo limechukua uhai wa Inspekta Peter Kigugu, F.3451 Koplo Francis, F.6990 PC Haruna, G.3247 PC Jackson, H.5503 PC Siwale, H.1872 PC Zacharia, H.7629 PC Maswi na H.7680 PC Ayoub, ni mwendelezo wa matukio mengine saba ya aina hiyo yaliyotokea katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja Mkoa wa Pwani.
Ingawa hadi sasa si Jeshi la Polisi wala mamlaka nyingine ambazo zimekwishaeleza kwa uwazi kiini cha kuwako kwa mfululizo wa matukio ya aina hiyo katika maeneo yale yale, lakini utekelezaji wake na aina ya watu wanaotekeleza unaelezwa kuwa na mwelekeo wa kigaidi.
Timu ya MTANZANIA Jumamosi ilifika katika eneo la tukio na baadaye Kituo cha Polisi Bungu iliposhuhudia gari aina ya Toyota Land cruiser lenye namba za usajili PT 3713, lililoshambuliwa na wahalifu likiwa lina jumla ya matundu 22 ya risasi.
Upande wa kioo cha mbele cha gari hilo lilikuwa na matundu tisa, wakati ubavu wa kushoto ukiwa na matundu mawili na upande wa kulia juu kulikuwa na tundu kubwa moja na upande wa nyuma kukiwa na matundu sita.
No comments:
Post a Comment