Katika hali isiyotarajiwa, baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita juzi walikataa kupokea msaada wa vyakula na sabuni kama zawadi ya sikukuu ya Pasaka, badala yake wakaomba wapelekewe dawa na vifaa tiba.
Tukio hilo lililoacha gumzo lilitokea wakati kikundi cha Huruma kinachoundwa na wanawake wajasiriamali Wilaya ya Bukombe kilipotembelea hospitali hiyo kugawa zawadi kwa wagonjwa.
Mmoja wa wagonjwa waliogoma kupokea zawadi hiyo, Lucia Mbalala alisema muda umefika kwa wanaoguswa kusaidia wagonjwa kwa kutumia fedha kidogo walizonazo kununulia vitu muhimu vitakavyosaidia matibabu ikiwamo dawa na vifaa tiba badala ya chakula.
“Inamfaa nini kumpa zawadi ya chakula na sabuni mgonjwa aliyelazwa hospitalini siku tatu bila kupata hata ya panadol? Lazima Watanzania tubadilike kimtazamo kwa kukataa zawadi zisizo na tija katika maisha na jamii yetu,” alisema Mbalala.
Alisema badala ya kusaidia, wengi wanaotembelea wagonjwa na watu wengine wenye uhitaji maalumu hulenga kujipatia sifa kisiasa au kwa malengo mengine yanayojificha nyuma ya zawadi hizo.
No comments:
Post a Comment