Darasa la saba 400 kuondolewa kazini Morogoro

Zaidi ya Wafanyakazi 400 wa Serikali wanatarajia kuondolewa kazini mkoani Morogoro kutokana na kushindwa kujiendeleza kielimu baada ya kuajiriwa miaka 13 iliyopita wakiwa na vyeti vya elimu ya msingi.
Watumishi hao ambao wengi wao ni wauguzi, wahudumu wa afya, madereva, wahudumu wa ofisi, watendaji wa mitaa, vijiji na kata tayari wamenyimwa mishahara yao ya mwezi huu.
Akizungumzia zoezi hilo aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Kimamba wilayani Kilosa, Mashaka Motile amesema katika wilaya hiyo watumishi zaidi ya 80 wamenyimwa mshahara bila maelezo yoyote na walipofuatilia ndipo walipofahamishwa kuwa walipewa muda wa kujiendeleza na wameshindwa kufanya hivyo.
“Hakuna barua yoyote tuliyopewa ya kusimamishwa kazi ila mshahara wa Julai hatujapewa na tulipofuatilia tuliambiwa kuna waraka wa Serikali unaosema wale wote walioajiriwa kuanzia mwezi Mei 20, 2004 wakiwa na elimu ya msingi na wameshindwa kujiendeleza wanatakiwa kuondolewa,” amesema.
Motile anasema yeye na baadhi ya watendaji wengine walisimamishwa kazi kimakosa kwani agizo linasema wasimamishwe kazi walioajiriwa kuanzia Mei 20, 2004 lakini wao waliajiriwa Mei Mosi, 2004.

No comments:

Post a Comment